1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamal Ganzouri atakiwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Misri

25 Novemba 2011

Imeripotiwa kwamba Baraza la Kijeshi la Misri limemteua Kamal al-Ganzouri kuwa waziri mkuu mpya lakini waandamanaji wanapinga na wanaendelea kukusanyika kwa maandamano dhidi ya utawala huo.

https://p.dw.com/p/13GvH
Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Misri, Hussein Tantawi
Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Misri, Hussein TantawiPicha: picture alliance/dpa

Kwa mujibu wa televiseni ya serikali nchini Misri, Ganzouri amekubali uteuzi huo, huku gazeti la serikali, Al-Ahram, likiandika katika mtandao wake kuwa Ganzouri ataunda serikali kabla ya uchaguzi wa hapo Jumatatu.

Lakini waandamanaji katika uwanja wa Tahrir wamezipokea taarifa za uteuzi huo kwa hasira, na kuapa kuendelea na maandamano yao hadi utawala wa kijeshi uondoke madarakani.

"Tulikuwa tumetarajia kuwa kila kitu kitakuwa kimetekelezwa katika kipindi cha miaka miwili baada ya mapinduzi, lakini kutoka mwezi Februari hadi Novemba, hatujaona matakwa yetu yakitimizwa. Ni karibuni mwaka mzima sasa, watu wanataka mabadiliko na wanauawa na bado hakuna matokeo kwa mapinduzi yao. Ndiyo maana tuna hasira. Hatumtaki Ganzouri wala Tantawi." Amesema mmoja wa waandamanaji hao.

Kama ilivyo kwa Tantawi, Ganzouri mwenye elimu ya uchumi, alihudumu kwenye utawala wa Hosni Mubarak akishikilia wadhifa huo huo wa uwaziri mkuu baina ya mwaka 1996 na 1999. Uteuzi huo ni hatua ya karibuni zaidi ya Baraza la Kijeshi kujaribu kuidhibiti tena nchi.

Jana, Baraza hilo liliomba radhi kwa vifo vya zaidi ya watu 40, ambao wameuawa na polisi tangu maandamano yaanze hapo Jumamosi. Jeshi limesema litachunguza mauaji hayo na pia litatoa fidia kwa familia za waliopoteza watu wao na majeruhi. Lakini mmoja wa viongozi wa Baraza hilo, Jenerali Mukhtar al-Mullah, amekataa wito wa waandamanaji wa kuondoka madarakani akisema ni lazima kwanza uchaguzi ufanyike.

"Ni lengo la kitaifa kwa Misri kufanya uchaguzi, majaji wako tayari, usalama upo tayari, na Wamisri lazima wawe tayari na wachukuwe dhamana ya kwenda kupiga kura. Hii ni hatua ya kwanza kujenga nchi ya kidemokrasia." Amesema Jenerali Mukhtar.

"Maandamano ya Watu Milioni Moja"

Katika picha hii ya mwaka 1997, Kamal Ganzouri (kushoto) akiwa na Rais Hosni Mubarak.
Katika picha hii ya mwaka 1997, Kamal Ganzouri (kushoto) akiwa na Rais Hosni Mubarak.Picha: picture-alliance/dpa

Hali ya usalama katika uwanja wa Tahrir ilikuwa tulivu hadi asubuhi ya leo, huku watu wakiendelea kukusanyika kwa ajili ya maandamano ya baada ya swala ya Ijumaa, waliyoyapa jina la "Maandamano ya Watu Milioni Moja".

Katika ujumbe wake uliotumwa kwenye ukurasa wa Facebook, Baraza la Kijeshi limesema kupitia muafaka uliosimamiwa na viongozi wa kidini, limefikia makubaliano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji kuacha mapambano.

Imamu mkuu wa Al-Azhar, Ahmed al-Tayeb, ametoa kauli kali zaidi dhidi ya Baraza la Kijeshi kuwahi kutolewa katika siku za karibuni, akisema kwamba muafaka hauwezi kuzaliwa kutoka dimbwi la damu.

"Majadiliano yoyote yanayolazimishwa kwa damu hayadumu na matunda yake ni machungu. Uongozi wa polisi na jeshi lazima utowe amri mara moja kwamba hairuhusiwi kuelekeza bunduki zao kwa waandamanaji, kwa sababu yoyote ile iwayo." Amesema Imam Ahmed.

Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ameielezea hali nchini Misri kuwa inatisha na amewataka watawala kuacha mara moja utumiaji wao wa nguvu dhidi ya waandamanaji.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP
Mhariri: Oummilkher Hamidou