Jumuiya ya kimataifa kuiwekea vikwazo Syria
30 Aprili 2011Kimsingi, Umoja wa Ulaya, umekubali kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya Syria. Nae Rais wa Marekani Barack Obama ameidhinisha vikwazo dhidi ya shirika la upelelezi la Syria na jamaa wa Rais wa Syria Bashar al-Assad.
Katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imewaonya raia wa Ujerumani kutosafiri kwenda Syria kwa sababu ya machafuko yanayozidi kushika kasi nchini humo. Vile vile Wajerumani walioko nchini humo, wameshauriwa kuondoka wakati ambapo bado inawezekana kufanya hivyo kwa usalama.
Wakati huo huo, nchini Syria, waandamanaji hiyo jana, walimiminika barabarani, baada ya sala ya Ijumaa. Vikosi vya usalama mara nyingine, vilitumia nguvu dhidi ya waandamanaji hao. Kwa mujibu wa shirika la haki za binadamu la Syria, takriban watu 48 wameuawa wakati wa maandamano katika sehemu mbali mbali nchini humo.