1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa ishikamane kuisaidia Pakistan

16 Agosti 2010

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kushikamana na kuisaidia Pakistan.Mwito huo umetolewa baada ya kuyatembelea maeneo yaliyoathirika kwa mafuriko nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/Oowe
In this photo provided by the United Nations, U.N. Secretary General Ban Ki-moon visits the Sultan Colony, an Internally Displaced Persons’ camp, in the Province of Punjab, near the city of Multan. Sunday, Aug. 15, 2010. Ban said Sunday he has never seen anything like the flood disaster in Pakistan after surveying the devastation and urged foreign donors to speed up assistance to the 20 million people affected. (AP Photo/United Nations, Evan Shneider)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki-moon akizungumza na wahanga wa mafuriko ya Pakistan.Picha: AP

Katibu Mkuu Ban Ki-moon alishtushwa na kuhuzunishwa na yale aliyoona alipotembelea maeneo yaliyoathirika kwa mafuriko nchini Pakistan.Alisema:

"Kamwe sitosahau uharibifu na mateso niliyoshuhudia leo hii. Nimezuru maeneo mengi yaliyoteketezwa kwa maafa ya kimaumbile, katika sehemu mbali mbali duniani. Lakini sijawahi kuona uharibifu kama huu.Jumla ya watu milioni 20 wameathirika."

Ban amewahamiza wafadhili wa kimataifa kuharakisha misaada na kuonya madhara zaidi baada ya asilimi 10 ya umma wa milioni mia moja na sabini nchini Pakistan kuathirika kwa mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa. Mamia ya vijiji vimezingirwa kwa maji,barabara zimebomoka na maelfu ya watu wamepiga kambi kando ya barabara wakiongojea kusaidiwa. Hadi watu 1,600 wameuawa na wengine milioni 2 wamepoteza makaazi yao huku hasira ikizidi miongoni mwao.Hali hiyo inahatarisha utulivu wa kisiasa, uchumi unaodorora na hata serikali isiyo maarufu na inayokabiliwa na uasi wa wanamgambo.

Serikali ya Pakistan imetuhumiwa kuwa imekawia kushughulikia maafa hayo na walionusurika,kwa sehemu kubwa wametegemea wanajeshi na mashirika ya misaada ya kigeni. Wachambuzi wanasema, Pakistan inayotazamwa kuwa ni nchi ambako ufisadi imekithiri na ziara iliyofanywa hivi karibunina Rais wa nchi hiyo Asif Ali Zardari barani Ulaya wakati wa maafa ya nchi yake, ni mambo yaliyowavunja moyo wafadhili wa kigeni.Hii leo mamia ya wahanga wa mafuriko hayo wameziba barabara karibu na eneo la Sukkur lililoathirika zaidi. Watu hao wanalalamika kuwa misaada inapelekwa pole pole na wanatendewa kama ni wanyama. Mmoja wao amesema kuwa vyombo vya habari vinapokuwepo ndio maafisa wa serikali huenda kugawa chakula.

Hali hiyo mbaya inayoendelea inatisha amesema, mkurugenzi wa shirika la misaada,Oxfam nchini Pakistan, Neva Khan. Jamii zinahitaji kwa dharura maji safi ya kunywa, mahala pa kujisaidia na mambo mengine ya kuhudumia usafi.Lakini msaada uliopo hivi sasa ni mdogo mno.Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, asilimia 25 tu ya msaada wa dola 459 uliohitajiwa hapo mwanzoni, ndio uliowasili. Hiyo ni tofauti na kiasi cha dola bilioni moja zilizotolewa na Marekani mwaka jana kwa mshirika wake Pakistan kuisaidia kupambana na wanamgambo nchini humo.

Mwandishi/Webermann,Jürgen/ZPR/P.Martin/RTRE/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman