Jumuiya ya Kiarabu bado kuomba uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.01.2012
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jumuiya ya Kiarabu bado kuomba uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imekubali kuruhusu timu ya waangalizi wake kubakia nchini Syria kumaliza kazi yao ya mwezi mmoja, na imejizuia kuomba uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa kama ilivyokuwa imefikiriwa mwanzo.

Waandamanaji wa Syria wakiandamana nje ya ukumbi wa mkutano wa Jumuiya ya Kiarabu.

Waandamanaji wa Syria wakiandamana nje ya ukumbi wa mkutano wa Jumuiya ya Kiarabu.

Uamuzi wa Jumuiya hiyo ulifikiwa jana mjini Cairo, huku kukiwa na maandamano nje ya ukumbi wa mikutano, kupinga kazi inayofanywa na timu ya waangalizi nchini Syria. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiarabu, Nabil Al-Arabi, alisema waangalizi wataendelea na kazi yao kwa uaminifu na kwamba Jumuiya yake itasubiri ripoti kamili tarehe 19 mwezi huu. Al-Arabi aliyasema hayo mara baada ya mkuu wa timu ya waangalizi, Mustafa al-Dabi, kuwasilisha ripoti ya awali ya timu yake.

Ingawa ripoti hiyo haijawekwa wazi, chanzo kimoja cha habari kimesema timu ya waangalizi imeziita lawama zinazoelekezwa kwake hazina uwiano. Ripoti pia inasema kwamba serikali ya Syria imekuwa ikiendeleza ukandamizaji dhidi ya waandamanaji. Katika sehemu nyengine ripoti hiyo inaishutumu serikali ya Syria kuwashikilia mahabusu katika maeneo yasiyofahamika.

Licha ya kuyabainisha yote hayo, upinzani nchini Syria umesema kwamba, kwa kuiruhusu timu ya waangalizi kuendelea na kazi zake, Jumuiya ya Kiarabu inaipa serikali ya Syria muda zaidi wa kuwauwa waandamanaji.

Viongozi wa Jumuiya ya Kiarabu wakikutana mjini Cairo.

Viongozi wa Jumuiya ya Kiarabu wakikutana mjini Cairo.

Akizungumza kutokea Uturuki alikokimbilia, mmoja wa viongozi wa upinzani Anas Abdeh, amesema ni lazima Jumuiya ya Kimataifa izuwie kumwagwa kwa damu ya Wasyria, vyenginevyo itakuwa sehemu ya ukatili huo.

"Tunataka kuiambia wazi Jumuiya ya Kiarabu, kwamba katika wakati huu ambapo hawaidhibiti serikali ya Syria, Wasyria wanaendelea kuuawa. Jumuiya ya Kiarabu inashiriki kwenye umwagaji damu huu."

Jana peke yake, watu 32 waliuawa kwa mujibu wa vyanzo vya upinzani. Taarifa za vifo hivi zimekuwa shida kuzithibitisha kwani serikali ya Syria hairuhusu waandishi habari kutoka nchi za kigeni. Wengi katika upinzani nchini Syria wamevunjwa moyo na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na wanataka Umoja wa Mataifa uingilie kati kumaliza umwagaji damu.

Baada ya mkutano huo hapo jana, Waziri Mkuu wa Qatar, Hamad al-Thani, alisema kwamba sasa ni wakati wa serikali ya Syria kuchukuwa hatua za uhakika kusimamisha ukandamizaji, akiongeza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitasubiri tena mapendekezo ya Jumuiya ya Kiarabu kuchukuwa hatua.

Alipoulizwa ikiwa hiyo inaamisha kuwa Umoja wa Mataifa utaingilia kati, alijibu hapana, ingawa alisema jalada la Syria liko kwenye meza ya Baraza la Usalama.

Kiongozi wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani

Kiongozi wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani

"Hatutaki kumtisha mtu yeyote. Tunajaribu kushirikiana na kila mtu hadi tufikie amani nchini Syria." Alisema Al-Thani.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana hapo kesho mjini New York, kulijadili suala la Syria, lakini wataalamu wanasema kwamba serikali za magharibi hazina matumaini ikiwa kutakuwa na hatua yoyote itakayopigwa. Urusi na China zimekuwa zikizuwia mapendekezo ya vikwazo dhidi ya serikali ya Syria, yanayoletwa kwenye Baraza hilo katika siku za hivi karibuni.

Kiasi ya waangalizi 160 wa Jumuiya ya Kiarabu wamesambazwa nchini Syria kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita, kuthibitisha ikiwa serikali inatekeleza masharti ya mpango wa amani wa Jumuiya hiyo, likiwemo la kuondosha vikosi vyake mitaani, kuachia wafungwa na kuruhusu vyombo vya habari kuripoti.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Hamidou Oummilkheir

DW inapendekeza

 • Tarehe 09.01.2012
 • Mwandishi Mohammed Khelef
 • Maneno muhimu Syria
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13gIL
 • Tarehe 09.01.2012
 • Mwandishi Mohammed Khelef
 • Maneno muhimu Syria
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13gIL

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com