1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joyce Banda achukuwa madaraka ya kuiongoza Malawi

Mohamed Dahman7 Aprili 2012

Makamo wa Rais wa Malawi Joyce Banda amechukuwa madaraka ya kuiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika Jumamosi (06.04.2012) kufuatia kifo cha Rais Bingu wa Mutharika.

https://p.dw.com/p/14ZLR
Joyce Banda Makamo wa Rais wa Malawi anayechukua madaraka ya Mutharika.
Joyce Banda Makamo wa Rais wa Malawi anayechukua madaraka ya Mutharika.Picha: Reuters

Maandalizi yako njiani katika bunge la Malawi kumuapisha Banda kushika wadhifa huo wa urais.

Hofu ya kuzuka kwa mapambano ya kuwania nafasi ya kumrithi rais huyo imeanza kupunguwa kutokana na asasi za kitaifa kuunga mkono makabidhiano ya madaraka kwa kuzingatia katiba.

Serikali imethibitisha rasmi kifo cha Mutharika mwenye umri wa miaka 78 hapo Jumamosi ikiwa ni siku mbili baada ya kufariki kwake kutokana na mshtuko wa moyo.

Mwili wake ulikuwa umepelekwa katika hospitali ya kijeshi nchini Afrika Kusini. Kuchelewa kutangazwa kwa kifo chake kulizusha hali ya wasi wasi juu ya kuwepo kwa mgogoro wa kisiasa kwa sababu Banda alikuwa ametimuliwa kutoka chama tawala cha Mutharika cha DPP hapo mwaka 2010 kufuatia mabishano juu ya mtu wa kumrithi rais juu ya kwamba aliendelea kushikilia wadhifa wake serikalini.

Marehemu Bingu wa Mutharika
Marehemu Bingu wa Mutharika.Picha: Reuters

Banda mwenye umri wa miaka 61 ambaye atakuwa mkuu wa nchi wa kwanza mwanamke katika eneo la kusini mwa Afrika alikuwa na mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Lilongwe ambapo alitangaza siku 10 za maombolezo rasmi ya Mutharika ambaye aliitawala Malawi kwa miaka minane. Ameamuru bendera za taifa kupepea nusu mlingoti na shirika la utangazaji la taifa kupiga muziki wa kuhuzunisha.

Ametowa wito kwa Wamalawi kuwa watulivu na kudumisha amani katika kipindi hiki cha maombolezo. Banda alikuwa akizungumza huku akiwa ameandamana na mwanasheria mkuu wa serikali na wakuu wa jeshi na polisi.

Katiba yaendelea kufanya kazi

Alipoulizwa na mwandishi wa habari iwapo alikuwa anachukuwa madaraka ya urais,Banda mwanaharakati wa haki za wanawake alijibu " kama unavyoona, katiba inafaya kazi".

Katiba inataja kwamba makamo wa rais anachukuwa madaraka iwapo rais amefariki lakini ilionekana kwamba Mutharika alikuwa akimuandaa mdogo wake Peter ambaye ni waziri wa mambo ya nje kuwa mrithi wake.

Banda anatazamiwa kuiongoza nchi hiyo hadi uchaguzi ambao umepangwa kufanyika hapo mwaka 2014. Ofisi ya rais na baraza la mawaziri vimetowa taarifa yenye kuwahakikishia raia na jumuiya ya kimataifa kwamba katiba ya Jamhuri ya Malawi itaheshimiwa ipasvyo katika kuongoza kipindi cha mpito.

Uingereza na Marekani ambazo zote mbili zilikuwa wafadhili wakuu wa Malawi hadi pale zilipositisha msaada wa mamilioni ya dola kutokana na mzozo na Mutharika juu ya sera zake na vitendo vyake, zimehimiza makabidhiano ya madarala yafanyike kwa utulivu kwa kuheshimu katiba.

A protester burns vegetation in a street in Lilongwe, Malawi, Wednesday, July 20, 2011. Protesters went on the rampage after a court injunction stopped them protesting the economic and democratic crisis in the country. A coalition of more than 80 rights groups had organised nationwide protest marches for Wednesday. They wanted to protest what they say are moves by the Malawi's President Bingu wa Mutharika to roll back hard-fought democratic gains made since the first democratic polls in 1994 removed dictator Kamuzu Banda from power. (Foto:Diane Boles/AP/dapd)
Ghasia za kupinga utawala wa Mutharika mjini Lilongwe.Picha: dapd

Dalili za huzuni ni ndogo

Mitaa ya mji mkuu wa Lilongwe na ile ya mji mkubwa wa kibiashara Blantyre ilikuwa kimya hapo Jumamosi juu ya kwamba polisi walikuwa wakilinda vituo muhimu.

Kulikuwa hakuna huzuni ya hadharani kuhusiana na kifo hicho cha Mutharika.Wengi wa wananchi milioni 13 wa Malawi walikuwa wakimuona kama dikteta na kuhusika binafsi katika mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo ambao umezidi kuchochewa na mzozo wa kidiplomasia na mkoloni wake wa zamani Uingereza mwaka mmoja uliopita.

Uingereza na nchi nyengine zilisitisha msaada wenye thamani ya asilimia 40 ya matumizi ya serikali na kusababisha kukosekana kwa mafuta na kupanda kwa bei za vyakula jambo ambalo lilipelekea machafuko ya umma na kushutumiwa kwa sera za kiuchumi za Mutharika na taasisi mbali mbali ikiwa ni pamoja na Kanisa Katoliki na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Wakati repoti za kifo chake zikianza kuzagaa katika mji mkuu kulikuwa na mripuko wa shangwe kutoka kwa watu waliobwia pombe ikiwa ni miongoni mwa wale wanaomshutumu Mutharika kwa kuirudisha miaka 18 nyuma demokrasia ya nchi hiyo inayojulikana kama "Moyo Mkunjufu wa Afrika".

Duru za matibabu zinasema mwili wa Mutharika ulisafirishwa Afrika Kusini kwa sababu matatizo ya nishati nchini Malawi ni makubwa mno kwamba hospitali ya taifa ya Lilongwe isingeliweza kuufanyia uchunguzi ipasvyo mwili wa marehemu au hata kuuweka mwili huo kwenye vipoza joto.

Banda amesema wakiwa kama serikali watashauriana na familia ya wafiwa, kushauri tarehe ya kurudi kwa rais wao huyo kutoka Afrika Kusini na maandalizi mengine ya mazishi.

Banda amewataka wananchi wote wa Malawi kuungana naye kuiombea roho ya marehemu ilazwe mahala pema.
Mwandishi: Mohamed Dahman /RTRE

Mhariri : Stumai George