1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Jeshi la Israel laanzisha operesheni kubwa ya ardhini Gaza

6 Desemba 2023

Mapigano makali yameendelea kuripotiwa katika Ukanda wa Gaza ambako Jeshi la Israel limetangaza kuwa kwa mara ya kwanza limeanzisha operesheni kubwa ya ardhini na wamefanikiwa kukizingira kabisa kitongoji cha Khan Younis

https://p.dw.com/p/4Zp76
Nahostkonflikt | Bodenoffensive der israelischen Armee im Gazastreifen
Wanajeshi wa Israel (IDF) wakiendesha operesheni ya ardhini huko GazaPicha: IDF/Xinhua/picture alliance

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limeielezea siku ya jana Jumanne kuwa "siku iliyoshuhudia mapigano makali zaidi" tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini katika Ukanda wa Gaza, yenye lengo la kuiangamiza Hamas ambayo imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya na mataifa kadhaa ya Magharibi kuwa  kundi la kigaidi.

Israel imeapa kuliangamiza kundi hilo la wanamgambo wa Kiislamu baada ya kufanya mashambulizi makubwa kusini mwa Israel ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuawa na wengine 240 kuchukuliwa mateka.

Wakati wito wa kuwalinda raia ukiendelea kutolewa, jeshi la Israel limewataka wakaazi kuhama kutoka sehemu za kusini mwa Gaza na kuelekea katika maeneo salama yaliyotengwa ili kuepuka mapigano hayo.

Soma pia:Israel yashambulia Khan Younis, kusini mwa Gaza

Mkuu wa shirika la Marekani la maendeleo na misaada ya kimataifa (USAID) Samantha Power amesema msaada mpya wa Marekani wa dola milioni 21 utatolewa kwa ajili ya watu wa Gaza, na msaada huo utaelekezwa katika sekta za usafi, makazi na chakula.

Nahostkonflikt | Bodenoffensive der israelischen Armee im Gazastreifen
Mashambulizi ya Israel yanaendelea katika Ukanda wa GazaPicha: IDF/Xinhua/picture alliance

Mtawala wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, amelaani kile alichokitaja kuwa ni  "aibu" ya kimataifa kuruhusu vita huko Gaza kuendelea. Wizara ya afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema kuwa vita hivyo hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 15,800 katika eneo la Palestina.

Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) walionukuliwa na mashirika ya habari ya AP na AFP wamesema makadirio yao ya idadi ya watu waliouawa Gaza ni sawa na yale yanayotolewa na Wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas na wamesisitiza kuwa wapiganaji 5,000 wa Hamas wameuawa.

Maonyo ya Umoja ya mashirika ya UNICEF na WHO

Lakini Umoja wa Mataifa umeonya kwamba haiwezekani kuunda kile kinachoitwa "maeneo salama" kwa raia katika Ukanda wa Gaza ili kukimbia mashambulizi ya Israel.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF James Elder , amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video kutoka mjini Cairo kwamba maeneo hayo yanayoitwa salama hayana mantiki, hayawezekani, na anadhani mamlaka inalifahamu hilo.

Still DW Interview James Elder
Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF James Elder Picha: DW

Elder ameendelea kuwa eneo huitwa salama pindi unapoweza kuwahakikishia watu hali ya chakula, maji, dawa na makazi, na kusisitiza kuwa kwa ameshuhudia mwenyewe kuwa yote hayo hayapo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya pia kwamba hali katika ardhi ya Palestina iliyozingirwa inazidi kuwa mbaya kadri muda unavyosonga mbele.

Soma pia: Juhudi za upatanishi kati ya Israel na Hamas zinaendelea

Richard Peeperkorn, mwakilishi wa WHO huko Gaza, amesema kunashuhudiwa mashambulizi makali ya mabomu yanayoendelea pande zote, ikiwa ni pamoja na maeneo ya kusini, Khan Younis na hata Rafah, huku akisisitiza kuwa msaada wa kibinadamu unaowasili Gaza ni "mdogo mno."

Peeperkorn amebainisha wazi kabisa kuwa tunashuhudia kwa sasa janga linaloongezeka la kibinadamu, na kusema shirika lao limeondoa maghala yake ya misaada kusini mwa Gaza, kufuatia "angalisho" kutoka kwa jeshi la Israel, taarifa iliyokanushwa na Tel-Aviv iliyosema kuwa haikuiamuru WHO kuondoa ghala zake mbili huko Khan Younis.