Kundi la CRG latoa ripoti ya mauaji ya halaiki Congo
18 Septemba 2017Ripoti hiyo mpya iliyotolewa na kundi la utafiti la CRG la chuo kikuu cha New York ndio ripoti ya kina na ya hivi karibuni juu ya mauaj ya zaidi ya watu 800, na ya kwanza inayotoa nadharia ya uhakika ya waliyodaiwa kutekeleza matukio hayo.
Ripoti hiyo imeandaliwa kufuatia mahojiano waliofanyiwa watu 249 wakiwemo wahalifu, watu waliyoshuhudia, waathiriwa pamoja na ripoti za ndani za Umoja wa Mataifa na rekodi ya watu waliyokamatwa kuhusika na mauaji hayo.
Inadaiwa milioni kadhaa waliuwawa Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kati ya mwaka 1996 na 2003 katika migogoro ya kikanda huku makundi ya wanamgambo wakiendelea kufanya kazi zao katika maeneo hayo. Lakini mauaji yaliyofanyika mjini Beni ndio yaliyokuwa mabaya na ya kushtua katika matukio ya hivi karibuni.
Kundi hilo la CRG limewanukuu baadhi ya mashahidi waliyosema makamanda wa kijeshi akiwemo aliyekuwa generali mkuu wa kanda hiyo aliunga mkono na hata kupanga mauaji. Katika baadhi ya mauaji hayo duru zimeliambia kundi hilo la CRG kwamba wanajeshi walizingira eneo ili wahanga wasiweze kutoroka.
Kwa upande wake msemaji wa serikali ya Congo Lambert Mende amesema maafisa kadhaa wa ngazi ya juu tayari wamehukumiwa kufuatia kuhusika katika mauaji hayo lakini pia akaikosoa ripoti ya CRG kwa kujaripu kufufua mambo ya zamani. Hata hivyo jenerali aliyetajwa katika ripoti hiyo Muhindo Akili Mundos,anaendelea kukanusha kuhusika binafsi katika mauaji hayo.
Huku hayo yakiarifiwa ripoti imetoa pendekezo la kufanyika uchunguzi zaidi huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitolewa wito wa kuwawekea vikwazo watu waliyohusika na machafuko yaliyotokea karibu na Beni.
Kulingana na ripoti ya CRG mauaji ya kwanza ya halaiki yalipangwa mwaka wa 2013 na viongozi wa zamani wa jeshi la Congo APC, mrengo wa waasi kutoka vita vya Congo mwaka wa 1998-2003 waliyokuwa wanajaribu kuidhoofisha serikali kuu.
Kwa sasa mauaji makubwa yamepungua Beni mwaka huu lakini wanajeshi kutoka serikali ya Congo na wale wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kupambana na makundi ya wanamgambo katika eneo hilo. Mmoja ya wanajeshi wa kulinda amani kutoka Tanzania aliuwawa na mwengine kujeruhiwa siku ya Jumapili baada ya mapigano ya wanamgambo. Hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa ujumbe wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa aliyezungumza na chombo cha habari cha Reuters.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu