1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Israel yaukaribisha mpango wa amani wa Waarabu

25 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBfK

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Misri, Abul Gheit, amesema Israel imeukaribisha mpango wa amani uliofufuliwa na jumuiya ya nchi za kiarabu.

Waziri Gheit ameyasema hayo leo mjini Jerusalem nchini Israel baada ya kufanya mazungumzo na mwenzake wa Jordan, Abdel Ilah al Khatib, rais wa Israel, Shimon Peres na waziri wa kigeni wa Israel, Tzipi Livni.

Waziri Livni amesema mpango wa amani wa Waarabu ni fursa ya kufikia amani baina ya Israel na Wapalestina.

´Naamini mpango wa amani wa Waarabu ni fursa ya kihistoria kwa mahusiano ya kiarabu lakini pia kwa mchakato mzima wa amani baina ya Israel na Wapalestina. Naamini ipo haja ya kuendeleza mchakato wa amani baina ya Israel na Wapalestina.´

Waziri Livni ameongeza kusema anaamini kuna umuhimu wa jumuiya ya nchi za kiarabau kuwasaidia Waisraeli na Wapalestina wachukue hatua zifaazo kuitimiza ndoto ya kuwepo mataifa mawili.

Mpango wa amani uliotayarishwa kwenye mkutano wa jumuiya ya nchi za kiarabu mjini Beirut nchini Lebanon mnamo mwaka wa 2002, unapendekeza kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Israel na mataifa yote ya kiarabu ikiwa Israel itaondoka kutoka maeneo inayoyakalia, kukubali kuundwa kwa taifa huru la Palestina na kutafuta suluhisho kwa tatizo la wakimbizi.

Ni mara ya kwanza kwa jumuiya ya kiarabu kutuma ujumbe wake kwenda Israel katika ziara iliyofanyika kufuatia ziara ya mjumbe wa pande nne zinazodhamini mpango wa kutafuta amani ya mashariki ya Kati, bwana Tony Blair.