1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jerome Champagne atawania urais wa FIFA

20 Januari 2014

Aliyekuwa naibu katibu mkuu wa FIFA Jerome Champagne ametangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais wa FIFA kuchukua nafasi ya Sepp Blatter. Champagne mwenye umri wa miaka 55 atawania katika uchaguzi wa 2015

https://p.dw.com/p/1AtsD
Picha: picture-alliance/Norbert Schmidt

Blatter aliiambia televisheni moja ya Ufaransa wiki iliyopita kuwa atatangaza kama atagombea tena uchaguzi wa rais au la, kabla ya mkutano mkuu wa FIFA mjini Sao Paolo mnamo Juni 10 na 11. Blatter mwenye umri wa miaka 77 amekuwa katika wadhifa huo tangu mwaka wa 1998.

Rais wa sasa wa Shirikisho la Soka barani Ulaya – UEFA, Michel Platini alisema mwaka jana kuwa atatangaza kama atagombea wadhifa wa urais wa FIFA au la, wakati wa Kombe la Dunia nchini Brazil au baada ya tamasha hilo ambalo linang'oa nanga Juni 12 hadi Julai 13.

Rousseff kukutana na Blatter

Huku ikiwa imesalia chini ya miezi mitano tu tukielekea nchini Brazil kwa dimba la Kombe la Dunia, Rais wa Brazil Dilma Rousseff atakutana na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani – FIFA Sepp Blatter pembezoni mwa Jukwaa la Kimataifa la Kiuchumi mjini Davos litakaloandaliwa wiki ijayo, ili kujadili kuhusu maandalizi ya tamasha hilo la soka ulimwenguni.

Viongozi hao wawili watakutana baada ya Blatter kuikosoa Brazil mapama mwezi huu kwa kujikokota katika maandalizi ya fainali za kombe la dunia, ikilinganishwa na mataifa mengine yaliyowahi kuandaa dimba hilo, katika kipindi cha miaka 16 ya uongozi wake. Aliwashutumu waandilizi wa Brazil kwa kuanza maandalizi wakiwa wamechelewa baada ya kupewa kibali cha kuwa mwenyeji wa kinyang'anyiro hicho mnamo mwaka wa 2007. Viwanja 6 kati ya 12 vitakavyotumiwa, havijatimiza muda wa mwisho uliowekwa na FIFA wa Desemba 31.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman