1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali McChrystal atimuliwa kazi

Sekione Kitojo24 Juni 2010

Afghanistan imeeleza masikitiko yake kuhusu kuondoshwa kwa kamanda wa majeshi ya Marekani ,ambaye amesifiwa kwa jitihada zake za kupunguza vifo miongoni mwa raia katika vita dhidi ya Walatiban.

https://p.dw.com/p/O1bw
Jenerali Stanley McChrystal, kamanda wa majeshi ya kimataifa nchini Afghanistan ambaye rais Obama amemwachisha kazi.Picha: AP

Afghanistan imeelezea masikitiko yake kuhusu kuondoshwa kwa kamanda wa majeshi ya Marekani, ambaye amesifiwa kwa jitihada zake za kupunguza vifo miongoni mwa raia katika vita dhidi ya Wataliban. Rais Barack Oabama alimuondoa Jenerali Stanley McChrystal katika wadhifa wake wa kuyaongoza majeshi ya Marekani na Jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Afghanistan baada ya kuukosoa mkakati wa utawala wake .

Akizungumzia hatua ya Rais Obama kumuondoa Jenerali McChristal kazini ,msemaji wa jeshi la Afghanistan Jenerali Zaher Azimi alisema , wangependelea kuona Jenerali McChrystal akibakia lakini uamuzi uliochukuliwa ni suala la ndani la Marekani. Rais Obama alimuondoa McChrystal jana na kumteuwa mkuu wake Jenerali David Patraeus kushika wadhifa huo. Petreaus ndiye aliyekua muasisi wa mafanikio katika vita vya Irak.

Vita hivyo vimefikia hali mbaya nchini Afghanistan, licha ya kuwapo kwa zaidi ya wanajeshi 150,000 kutoka nchi mbali mbali , na Taliban wakiwa katika ufanisi mkubwa tangu kuangushwa kwa utawala wao mwaka 2001.

Mwezi huu wa Juni tayari umekuwa mwezi ambao vifo vingi vimetokea kwa wanajeshi wa kigeni, ambapo vifo vya wanajeshi wanne katika ajali ya gari jana Jumatano vimefikisha idadi ya watu 75 kuuwawa.

Zaidi ya wanajeshi 300 wa majeshi ya kigeni wameuwawa nchini Afghanistan mwaka huu, ikilinganishwa na wanajeshi 521 kwa mwaka mzima ulipita, kwa mujibu wa tovuti ya icasualties.org. Wapiganaji wengi zaidi wameuwawa, lakini raia kadha pia wameuwawa, wengi wao katika mashambulio ya mabomu ya Wataliban, lakini wengine pia wameuwawa wakati majeshi ya kimataifa yakipambana na Wataliban pamoja na mashambulio ya anga ambayo hayakupata uelekezi sahihi.

Mkakati wa MacChrystal wa kupambana na wapiganaji una lengo la kuwashambulia Wataliban pale ambapo wamejizatiti zaidi, katika ngome yao kuu katika jimbo la Kandahar, na wakati huo huo kuimarisha usalama huku kukiwa na msukumo wa kujenga serikali ya kiraia na maendeleo. Wakati akitoa tamko la kumwachisha kazi jenerali McChrystal , rais Barack Obama amesisitiza kuwa hakuna tofauti za kisera na jenerali huyo.

"Sichukui uamuzi huu kutokana na tofauti za kisera na jenerali McChrystal, kwa kuwa tunakubaliana kikamilifu juu ya mkakati wetu. Na pia sitoi matamshi haya kutokana na hisia za kudharauliwa. Jenerali McChrystal amekuwa wakati wote akionyesha heshima kubwa na kutekeleza amri zangu kwa uadilifu."

Petraeus, kama kamanda wa majeshi ya Marekani nchini Iraq , alimwagiwa sifa kwa kiasi kikubwa kwa kubadilisha wimbi la mauaji katika nchi hiyo kwa kuweka msukumo wa kuboresha utawala wa kiraia pamoja na maendeleo.

Wakati akiwa ana wafuasi wengi katika utawala wa Marekani pamoja na uidhinishaji wa haraka unaotarajiwa katika baraza la seneti , jukumu lake muhimu litakuwa kuweka uhusiano mzuri na rais wa Afghanistan Hamid Karzai.

Tangu pale McChrystal alipochukua uongozi mwezi Juni mwaka jana ameweza kujenga uhusiano mzuri na Karzai, akitangulizana nae katika ziara zake kadha nchini humo katika juhudi za kuonyesha kuiunga mkono serikali yake.

Rais wa Afghanistan , ameeleza masikitiko yake kwa kuondoka McChrystal, amesema msemaji wa rais huyo.

Tulitumai kuwa haya hayatatokea, lakini uamuzi uliochukuliwa , tunauheshimu, amesema msemaji wa rais Waheed Omar. Akaongeza kuwa serikali inatarajia kutoa ushirikiano mzuri na mtu aliyechukua nafasi yake.

Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE

Mhariri: Mtullya abdu