1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za Umoja wa Ulaya kuleta utulivu Libya?

Saumu Mwasimba
17 Desemba 2017

Jumuiya ya Kimataifa itafanikiwa kumshawishi jenerali Khalifa Haftar kuunga mkono juhudi za amani na kuridhia mchakato wa kisiasa kuleta utulivu nchini Libya,hakuna mwenye jibu thabiti

https://p.dw.com/p/2pVN3
EU Kommission Brüssel
Picha: EU/M.Bottaro

Je wasuluhishi wa kimataifa wanaweza kumshawishi jenerali wa kijeshi nchini Libya Khalifa Haftar kwamba mustakabali wake utakuwa bora zaidi atakapokubaliana nao kuliko atakapokuwa hayuko upande wao? Hilo ni suala ambalo wanajiuliza wachambuzi wanaoifuatilia hali nchini Libya.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini sambamba na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wanataka kuwaokoa watu waliokwama katika vituo hatari kabisa vya kuwashikilia  wakimbizi nchini Libya. Umoja wa Ulaya umetowa yuro milioni 100 kwa washirika wake,shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na lile linaloshughulikia wakimbizi UNHCR kwa ajili ya kuunga mkono shughuli hiyo nchini Libya.

Lengo la jopo kazi hilo nchini Libya linaweza kuangaliwa kama ni hatua ya ushindi wa pande zote mbili chini ya mazingira magumu kabisa. Raia hao wanaoshikiliwa katika vituo maalum nchini Libya wanaweza kutumia mpango huo wa msaada wa kifedha wa Jumuiya ya Kimataifa kurudi makwao hali ambayo bila shaka itawaumiza kutokana na juhudi zao za kutafuta maisha bora kushindwa lakini angalau hawatolazimika tena kuteseka na kunyanyasika kama ilivyoonekana katika matukio yaliyoorodheshwa na shirika la kutetea haki za binadamu pamoja na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.

Libyen Europa Migration Zustände in Flüchtlingslagern
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Brabo

Wakati huohuo Umoja wa Ulaya unapunguza idadi ya wahamiaji wanaowasili katika pwani za Itali. Ingawa mgogoro wa wahamiaji sio tatizo pekee na pengine hata sio changamoto kubwa zaidi inayoikabili Libya kwa sasa. Siku kadhaa zijazo zitabaini ikiwa jungu linalotokota muda mrefu la vurugu  na mivutano ya kisiasa litaripuka. Makubaliano ya kisiasa ya Libya  yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa,ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa yaliyofikiwa Desemba 17 mwaka 2915 yanaelekea kufikia muda wake wa mwisho wa miaka miwili. Makubaliano hayo hata hivyo hayajawahi kutimizwa.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyopendekezwa katika makubaliano hayo haikuwahi kuzingatiwa.Fayez Mustafa al-Serraj aliyetajwa katika makubaliano hayo kama kiongozi wa baraza la rais la Libya na waziri mkuuu wa serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa GNA mpaka sasa hana mamlaka yoyote,na hana udhibiti wa nchi nzima. Wadau wengi wanataraji kwamba tarehe ya kumalizika kipindi cha makubaliano hayo kitapita bila ya kushuhudiwa tukio lolote na kuonekana kama hatua inayokumbusha kwamba uongozi wa kisiasa nchini humo bado umegawika na umekumbwa na mivutano.

Lakini kwa hakika matarajio hayo tayari yanaonekana kutokuwa na nafasi kubwa na yanategemea kwa kiwango kikubwa hatua zitakazochukuliwa na jenerali kamanda wa jeshi la taifa Khalifa Haftar ambaye anayashikilia mamlaka ya eneo zima la Mashariki mwa Libya akijiwekea makao makuu yake mjini Bengazi.Jenerali huyo amekataa kabisa kuiunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa au GNA kama inavyoitwa. Haftar aliwahi zamani kuwa rafiki na baadae adui wa kiongozi wa Libya aliyekuja kuondolewa madarakani Moammer Ghaddafi. Na sasa wafuasi wa jenerali huyo wanamtaka ajitangaze rais wa Libya.

Libyen Tripolis Fayez Serraj Einheitsregierung Treffen
Picha: picture-alliance/AP Photo/GNA Media

Vyombo vya habari Libya vimeonesha jinsi wafuasi wa Hifter wanavyoandamana dhidi ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka ujao chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa,wakiitumia siku ya leo 17.Desemba kama siku ya kukusanyika kupaza kilio chao cha kumtaka mbabe huyo wa kivita kutwaa hatamu. Mchambuzi wa kujitegemea Mary Fitzgerald ambaye ameishi Libya kwa miaka kadhaa anasema kuna wasiwasi mkubwa kuhusu nini kinachoweza kutokea katika tarehe hii.

Mchambuzi huyo anamuelezea Jenerali Haftar kama kizingiti kikubwa kuelekea maridhiano. Anasema jenerali huyo na washirika wake wameshazungumzia kuhusu jinsi walivyowapa wanasiasa wa Libya muda wa mwisho  na endapo watashindwa kufikia chochote basi vikosi vyake vitalazimika kuingia.Vikosi hivyo vitaingia wapi na kufanya nini hilo ndilo suali kubwa hivi sasa. Juhudi za Jumuiya ya kimataifa za kumfanya Hifter kuwa sehemu ya mpango wa kusaka amani zimemfanya Jenerali huyo kutoa kauli kadhaa akiahidi kujitolea kuunga mkono mchakato wa kisiasa kwa njia ya usawa na amani lakini hilo katu halijazikomesha vurugu katika mitaa ya Libya.

Libyen General Khalifa Haftar
Picha: picture alliance/dpa/M. Elshaiky

Elie Abouaoun ambaye ni mkurugenzi wa masuala ya Mashariki ya kati na Afrika Kaskazini katika taasisi ya amani ya Marekani amesema kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kutambua kwamba ulifanya kosa kubwa toka mwanzo kwa kushindwa kumjumuisha jenerali hiyo katika mchakato huo wa amani ingawa kuna wengine vile vile wanaohisi kwamba hakuna choche kizuri kinachoweza kufungamanishwa na jenerali Haftar na zaidi ni mtu anayestahili kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai ICC na sio kupewa fursa ya kuwa sehemu ya serikali ya Libya.

Mwandishi:Teri Schultz/Saumu Mwasimba

DW - Brussels.

Mhariri:John Juma