1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamii yakuwa mno nchini Uganda

Arndt, Corinna/ Dreyer, Maja27 Machi 2008

Hakuna maeneo mengi mengine duniani ambapo idadi ya wananchi inakua kwa kasi kama katika nchi za Kiafrika zilizo kusini kwa jangwa la Sahara. Uganda ni mfano mmojawao.

https://p.dw.com/p/DVn3
Hao wana bahati. Watoto wengi nchini Uganda hawawezi kwenda shulePicha: Achim Pohl/Das Fotoarchiv

Nchini Uganda kwa sasa ina wakaazi millioni 30, lakini idadi hii inakua kwa asilimia 3.2 kila mwaka. Kwa hivyo, baada ya miaka 20 idadi ya ujumla itakuwa mara mbili kubwa kuliko leo.


Katika kijiji cha Gwara-Gwara, kijiji kidogo kilicho mbali na barabara kuu akinamama hapa pamoja na watoto wao wachanga wanamsubiri Bibi Robina Abalo. Ni jambo lisilo la kawaida kwa mtu wa shirika la Uganda linalotoa huduma za kupanga uzazi kuja hapa Gwara-Gwara. Bi Abalo anazungumzia mimba inayotakiwa na isiyotakiwa, hatari za kuzaa na dawa za kuzuia mimba.


Kwa wastani, kila mwanamke wa Uganda anazaa watoto saba. Na kati ya wanawake wanne mmoja tu anatumia njia za kujikinga mimba. Kama anavyoeleza Bi Abalo, wengi hawana njia za kununua hizo dawa au condoms au wana hofu fulani, kwani kuna uvumi mwingi.


Bi Abalo anaeleza kwamba wanawake wanaamini kwamba watazaa watoto wenye ulemavu, watoto wasio na kichwa au wasiokuwa na miguu na kadhalika. Na anaendelea kusema: "Wanaume wanawashuku wake wao kwamba wanataka kutokuwa waaminifu lakini bila ya kutiwa mimba. Ni haya tunayoyapiga vita. Ikiwa wanawake wanakuja kwetu si jambo la kutokuwa waaminifu bali ni jambo la kuishi na kufa."


Kila siku nchini Uganda, wanawake 16 wanakufa baada ya kuzaa. Pia idadi ya watoto wachanga wanaokufa mapema ni kubwa mno. Hata hivyo, jamii inakuwa kwa haraka sana. Shule zimejaa, vilevile hospitali na umaskini ambao tayari ni mbaya unaenea zaidi. Bado lakini katika dini za Uganda, watoto ni baraka, ni sehemu ya utariji wa familia.


Asimilia 40 ya wanawake wa Uganda wanataka kuwa na watoto wachache tu, wengi wao lakini hawajui vipi kufanya hivyo, kwa sababu hawana ujuzi huu au kwa vile hawawezi kupata ushauri wala dawa za kujikinga na mimba.


Tatizo la ukuaji wa jamii za Kiafrika kwa muda wa miaka 10 iliyopita lilisahauliwa katika sera za misaada ya maendeleo kwa bara la Afrika. Fedha zinapatikana katika kupambana na ukimwi, lakini katika suala la mpango wa uzazi ni vigumu kugharamia miradi. Tangu hivi karibuni tu, nchi fadhili zimefahamu kwamba ongezeko kubwa la wananchi barani Afrika litapunguza faida za misaada ya maendeleo na ukuaji wa uchumi.


Fred Mafabi hahitaji kuelemishwa hayo yote. Tunakutana naye katika kijiji cha Namachere karibu na mlima Elgon. Anamiliki ngombe wawili na mbuzi watatu lakini hana ardhi ya kutosha ya kuwalisha. Yeye ameamua kitambo kutopata watoto wengine: "Tatizo ni wazi kabisa kama watoto hawawezi kwenda kusoma wala hawana chakula cha kutosha. Wazazi wangu walikuwa na watoto 30. Chukua mimi tu kama mfano na hali yangu ya maisha. Sikuweza kwenda shule. Ningekuwa na fursa, bila shaka maisha yangu yangekuwa bora kuliko yalivyo. Mimi nina watoto watatu tu, na basi. Hawa wote watatu wataenda shule."