1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

J3 0809 News

8 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBRg

Sydney. Viongozi wa APEC waidhinisha makubaliano ya kupunguza ujoto duniani.

Viongozi 21 wanaokutana katika mkutano wa ushirikiano wa mataifa ya Asia na Pacific mjini Sydney nchini Australia wametia saini makubaliano yenye lengo la kupunguza kasi ya kuongezeka kwa hali ya ujoto duniani.

Waraka huo wa makubaliano unatoa wito wa kuchukuliwa hatua za muda mrefu za kupunguza gesi zinazoharibu mazingira.

Miongoni mwa mambo mengine makubaliano hayo, yanatoa wito wa kupunguzwa matumizi makubwa ya nishati , ama kiwango cha nishati kinachohitajika katika ongezeko la ukuaji wa uchumi , kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo maamuzi haya pamoja na malengo mengine yaliyomo katika taarifa hiyo hayazilazimishi nchi wanachama kuyatekeleza.

Mwenyeji wa mkutano huo waziri mkuu wa Australia John Howard amesema kuwa makubaliano hayo yanaonyesha nia thabiti ya kundi hilo la mataifa kutaka kushughulikia suala la ongezeko la ujoto duniani na wakati huo huo kutoa nafasi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi.

Waziri mkuu Howard amesema kuwa makubaliano ya Sydney yameweza kuidhinishwa na anafikiri kuwa kwa viongozi wa nchi za APEC ni hatua muhimu sana kuelekea katika makubaliano ya hali ya hewa, ambayo yanatambua sio tu ukuaji wa uchumi bali hali mbali mbali katika ushughulikiaji wa suala la mabadiliko ya hali ya hewa.