1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Israel yatangaza kupanua operesheni zake Gaza

20 Novemba 2023

Israel imetangaza kuwa inalenga kupanua operesheni zake za kijeshi dhidi ya kundi la Hamas huko Gaza, na wapatanishi wa Qatar wamesema wanakaribia kufikia makubaliano yatakayopelekea kuachiwa huru kwa baadhi ya mateka.

https://p.dw.com/p/4ZAb7
Israelische Angriffe zielen auf das Al-Bureij-Lager im Zentrum von Gaza
Mtoto wa Kipalestina akishuhudia uharibifu mkubwa baada ya shambulio la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Al-Bureij huko Deir Al-Balah huko Gaza: 05.11.2023Picha: Adel Al Hwajre/ZUMA/picture alliance

Jeshi la Israel limesema linalenga kupanua vita vyake dhidi ya kundi la Hamas hadi kwenye maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza. Wizara ya afya huko Gaza imeeleza leo kuwa  shambulizi la Israel kwenye Hospitali ya Indonesia karibu na kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa ukanda huo, limesababisha vifo vya watu 12, wakiwemo wagonjwa, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. Jeshi la Israel limesema kuwa Jabalia ni miongoni mwa maeneo yanayozingatiwa kwani "wanawalenga magaidi na kushambulia miundombinu ya Hamas".

Kulingana na Wizara hiyo inayodhibitiwa na Hamas, hadi sasa watu 13,000 wakiwemo maelfu ya watoto tayari wameuawa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi baada ya shambulio la kigaidi la Hamas la Oktoba 7 lililosababisha vifo vya watu 1,200 na mateka 240 wakichukuliwa mateka.

Gaza Angriffe
Moshi ukitanda baada ya shambulizi la Israel katika hospitali ya Indonesia karibu na kambi ya Wakimbizi ya Jabalia: 12.11.2023Picha: Fadi Alwhidi/Anadolu/picture alliance

Wapatanishi wa Qatar wamesema jana Jumapili kuwa mazungumzo juu ya makubaliano ambayo yangewezesha kuachiliwa huru baadhi ya mateka yanaendelea, lakini kwa sasa yanakabiliwa na changamoto ndogo za kiutendaji, ingawa hakuna maelezo zaidi wala ratiba iliyotolewa, huku Israel na Hamas wakijizuia kuzungumzia mpango huo.

Viongozi wa mataifa ya kiarabu ziarani nchini China

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya kiarabu kutoka Mamlaka ya Palestina, Misri, Saudi Arabia, Jordan, Indonesia na wawakilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislam, wamefanya mikutano leo Jumatatu huko Beijing kuhusu mzozo huo, ambapo mwenzao wa China Wang Yi amesema taifa hilo lina nia ya kusaidia kurejesha amani katika Mashariki ya Kati na kwamba ni lazima ulimwengu "uchukue hatua za haraka kukomesha maafa ya kibinadamu" huko Gaza.

Soma pia: WHO yaitaja hospitali ya Al Shifa kama "eneo la kifo"

"Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kuzuia janga hili kuenea. Tangu kuzuka kwa mzozo huo, China imesimamia kidete suala la haki katika mzozo huu. Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii ili kuzuia kupanuka kwa mzozo, kulinda usalama wa raia, kuongeza usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kuzuia maafa ya kibinadamu. Tunatoa wito wa kurejea kwenye suluhisho la Serikali mbili na kufikiwa haraka iwezekanavyo kwa suluhu la kina, la haki na la kudumu kwa suala la Palestina."

China Peking | Außenminister Wang Yi trifft Vertreter Arabischer Länder
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi (Wa nne kutoka kushoto-mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na wenzake kutoka Mataifa ya Kiarabu na Kiislamu wakati wa mkutano mjini Beijing ili kuzungumzia mzozo wa Mashariki ya Kati: 20.11.2023Picha: Pedro Pardo/AFP/Getty Images

Ufaransa imetangaza kuwa itatuma mapema wiki hii helikopta eneo la mashariki mwa Mediterania ili kutoa msaada wa kimatibabu katika Ukanda wa Gaza. Ofisi ya Rais Emmanuel Macron imesema helikopta ya Dixmude ina uwezo wa kuwapokea wagonjwa 40 na itakuwa ikitoa huduma kwa watu walioathirika zaidi.

Soma pia: Maafisa wa Palestina kuizuru China juu ya mzozo wa Hamas na Israel

Serikali ya Japan kupitia Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Hirokazu Matsuno imesema mapema leo kuwa "inalaani vikali" kitendo cha meli yake ya "Galaxy Leader "kutekwa nyara na Wahouthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran katika Bahari Nyekundu. Japan imetoa wito kwa waasi, huku ikitafuta usaidizi wa mamlaka za Saudia, Oman na Iran ili hatimaye meli hiyo na wafanyakazi wake waachiliwe mara moja.