Israel yashambulia vituo katika Ukanda wa Gaza
5 Septemba 2010Mtu mmoja aliuawa na wengine watatu walijeruhiwa katika mashambulio mawili dhidi ya njia inayopitia chini kwa chini kuelekea Misri ambayo hutumiwa kwa biashara haramu.
Shambulio la tatu lililenga ngome ya zamani ya kundi la Hamas katika mji wa Khan Yunis ulio kusini mwa Ukanda wa Gaza. Jeshi la Israel limethibitisha kufanya mashambulio hayo.Imechukua hatua hiyo kujibu mashambulio mapya ya makombora yaliyolenga makaazi ya Wayahudi hivi karibuni kutoka kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Siku ya Alkhamisi Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas, walikutana ana kwa ana kwa mazungumzo ya amani mjini Washington. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutana ana kwa ana baada ya majadiliano ya amani kuvunjika takriban miaka miwili iliyopita.