1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kushambulia Ukanda wa Gaza

P.Martin21 Mei 2007

Israel ikiendelea kushambulia Ukanda wa Gaza, waziri wake wa miundo-mbinu ya taifa amesema, viongozi wote wa Hamas wapaswa kuuawa ili kuzuia makombora yanayovurumishwa na wanamgambo wa Kipalestina kusini mwa Israel.

https://p.dw.com/p/CHE5
Jengo lashika moto Gaza baada ya kushambuliwa na Israel
Jengo lashika moto Gaza baada ya kushambuliwa na IsraelPicha: AP

Mashambulio yaliyofanywa na Israel hii leo, yalilenga ngome ya Hamas kwenye Ukanda wa Gaza. Kwa mujibu wa maafisa wa Kipalestina,mtu mmoja aliuawa katika duka la mwashi wa kuchonga mawe. Israel lakini imesema,duka hilo lilikuwa likitengeneza maroketi.Shambulio hilo la Israel limefanywa siku moja baada ya kuuawa kwa Wapalestina 8 ambao hawakuwa shabaha.Shambulio hilo lililenga nyumba ya mwanasiasa wa chama cha Hamas,Khalil al-Hayya ambae wakati huo hakuwepo nyumbani;miongoni mwa wale waliouawa,sita walikuwa jamaa zake.Kwa mujibu wa Hamas,wawili tu ndio walikuwa wanamgambo wake.Chama cha Hamas ambacho,mara ya mwisho kilifanya shambulio la kujitolea muhanga nchini Israel mwaka 2004,kimetishia kulipiza kisasi.

Kwa upande,mwingine Waziri wa Miundombinu ya taifa,wa Israel,Binyamin Ben-Eliezer alipozungumza kwenye Redio ya Israel alisema,yeye hatofautishi kati ya wale wanaovurumisha makombora kuishambulia Israel na wale wanaotoa amri ya kufanya mashambulio yenyewe.Wakati huo huo waziri wa usalama wa ndani,wa Israel,Avi Dichter hii leo alisema,kiongozi wa Hamas alie uhamishoni nchini Syria,Khalid Meshaal,hatokuwa na kinga dhidi shambulio la Israel. Amesema, kiongozi huyo ni shabaha halali.Akaongezea kuwa hata waziri mkuu wa Wapalestina Ismail Haniyeh wa chama cha Hamas anaeishi Gaza,anaweza pia kulengwa ikiwa ni miongoni mwa wale wanaotoa amri ya kuishambulia Israel kwa maroketi.Haniyeh vile vile mwaka 2004 alipona chupu chupu,Israel iliposhambulia Ukanda wa Gaza na kumuua kiongozi wa kidini,Sheikh Ahmed Yassin.

Tangu Israel kuanza mashambulizi yake juma lililopita katika Gaza,si chini ya Wapaelstina 20 wameuawa,wengi wao wakihusika na chama cha Hamas.Israel imekituhumu cha Hamas kwa machafuko ya hivi sasa,na kwamba kinaelekeza hasira zake kwa Israel badala ya kushughulikia mgogoro wake na chama cha Fatah chenye siasa za wastani.