1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel haijaamua kuishambulia Iran

10 Novemba 2011

Israel imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zinazofaa kusimamisha mpango wa Iran wa kutengeneza silaha za atomiki, msimamo unaoonekana laini kidogo kuliko ule uvumi kuwa ingeliishambulia nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/138Dk
Rais Mahmoud Ahmadinejad akitembelea vinu vya kurutubisha madini ya yuraniam vya Natanz.
Rais Mahmoud Ahmadinejad akitembelea vinu vya kurutubisha madini ya yuraniam vya Natanz.Picha: AP

Ripoti iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema ugunduzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) unahakikisha kile ambacho wamekuwa wakikiamini kwa muda mrefu, kwamba malengo ya Iran ni kupata silaha za atomiki.

Ofisi hiyo ilisema umuhimu wa ripoti mpya ya IAEA ni kuwa sasa ulimwengu unapaswa kuchukua hatua za haraka kukomesha malengo hayo ya Iran, ambayo Israel inasema ni hatari kwa usalama wa eneo la Mashariki ya Kati na wa dunia nzima.

Uvumi ulienea wiki iliyopita kuwa Israel ilikuwa ikijiandaa kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran, lakini sasa inaonekana mkakati wa nchi hiyo ni kuungana na msimamo wa Marekani na nchi nyingine za magharibi, wa kukaza vikwazo dhidi ya Iran hadi pale itakapoachana na mpango wake huo.

Hata hivyo, kama alivyosema waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak, hatua zozote zinawezekana kushughulikia Iran na mpango wake.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud BarakPicha: dapd

''Msimamo wetu haujabadilika, na ninaamini hautabadilika. Tunaamini kuwa Iran haipaswi kuruhusiwa kumiliki silaha za nyuklia. Naamini huu pia ni msimamo wa Marekani na nchi nyingine za Ulaya. Nafikiri hatua za aina nyingi zinapaswa kuchukuliwa na hakuna mbinu inayoondolewa kwenye meza. Huo ndio msimamo wetu na sidhani kama kuna hatua yoyote ya haraka itakayochukuliwa sasa kuliko hayo niliyosema.'' Alisema Barak kuhusiana na msimamo wa Israel.

Lakini mpango wowote wa kuishambulia Iran kijeshi, au azimio lolote kupitia Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo zaidi kwa nchi hiyo vimepingwa vikali na Russia na China, nchi mbili zenye kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel, Tzipi Livni, alisema nchi hizo sasa hazina sababu ya kuzuia vikwazo dhidi ya Iran, kwa sababu sasa ushahidi wa dhamira yake upo.

''Nilipokuwa nikizungumza na viongozi wa Russia na China walisema hakuna sababu zinazoweza kuchukuliwa kwa vile hakuna ushahidi. Ushahidi huo sasa umepatikana. Kuna aina ya vikwazo ambavyo havikutekelezwa na sasa ni wakati wa kufikiria kwa makini. Muda ni kitu muhimu sasa, kwa sababu tunavyochelewa katika mazungumzo, wao wanakaribia lengo lao la silaha za nyuklia.'' Alisema Livni.

Nchini Marekani, bado kuna mgawanyiko kati ya serikali ya Rais Barack Obama juu ya hatua ya kuchukuliwa. Wakati wabunge wanaoiunga mkono Israel wanahimiza uwezekano wa kuishambulia kijeshi Iran, serikali inapendelea ushirikiano na washirika wao katika kulitatua suala la silaha za atomiki za Iran.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/IPS
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman