1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD:Tume ya uchaguzi yafanya maandalizi ya uchaguzi

14 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CG1N

Maafisa wa Tume ya uchaguzi nchini Pakistan wanakutana hii leo ili kukamilisha maandalizi ya uchaguzi wa wabunge unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Januari ijayo.Rais Pervez Musharraf wa Pakistan alitangaza tarehe hiyo baada ya shinikizo kufuatia kutangazwa kwa hali ya hatari mwanzoni mwa mwaezi huu.Vyama vya upinzani vinatisha kususia uchaguzi huo kwani hautakuwa na maana yoyote ikiwa hali ya hatari bado inadumishwa.

Tarehe haswa ya uchaguzi itatangazwa baada ya kuvunjwa kwa bunge hapo kesho aidha serikali za mikoa ifikapo tarehe 20 mwezi huu.Kwa mujibu wa katibu wa tume ya Uchaguzi Kanwar Dilshad mkutano huo unalenga kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika katika mazingira ya haki,huru na uwazi.

Wakati huohuo mwanasiasa wa upinzani na mcheza kriketi maarufu wa zamani Imran Khan anazuiliwa na polisi baada ya kutoka alikojificha.Mwanasiasa huyo alipanga kuhudhuria mkutano wa hadhara ili kupinga hali ya hatari iliyotangazwa,.

Kwa upande mwingine Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto yuko katika harakati za kuungana na wanasiasa wengine wa Upinzani ili kupinga sheria ya Rais Musharraf,.Bi Bhutto anatoa wito wa kujiuzulu kwa kiongozi huyo aidha kutangaza kutoshirikiana na Rais Musharraf katika serikali moja.

Marekani iliyo mwandani wa Pakistan hasa katika vita dhidi ya ugaidi inapanga kumtuma Islamabad Naibu Waziri wa mambo ya kigeni John Negroponte.Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanatoa wito kwa Marekani kumshinikiza Rais Musharaf.T Kumar ni mkurugenzi wa Shirika la Amnesty International tawi la Asia na Pacific mjini Washington anasema''Sisi Amnesty International pamoja na mashirika mengine 11 makubwa ya kutetea haki za binadamu tunadai kuwa Pakistan isitishiwe misaada ya usalama zikiwemo huduma za kijeshi mpaka pale Rais Musharraf atakapobatili sheria ya hali ya hatari na kuwaachia wanasheria wakuu''