1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Islamabad. Bomu lauwa watu 15.

2 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/CBKx

Nchini Pakistan , mlipuko uliotokea katika kituo cha upekuzi cha polisi umesababisha vifo vya watu 15 na kuwajeruhi wengine 22 katika mji wa Bannu katika eneo la wenyeji kaskazini magharibi ya mpaka na Afghanistan.

Polisi wamesema kuwa mtu aliyefyatua bomu hilo alikuwa amevalia nguo za mwanamke. Jeshi la Pakistan limetupilia mbali ripoti za hapo kabla kuwa mshambuliaji huyo alikuwa anajaribu kulenga mlolongo wa magari ya kijeshi. Mlipuko huo uliotokea jana Jumatatu ni wa hivi karibuni kabisa katika wimbi la mashambulizi yanayolengwa dhidi ya maafisa wa Pakistan tangu pale majeshi ya nchi hiyo yalipovamia msikiti mwekundu wenye mahusiano na kundi la kigaidi la Al – Qaeda mjini Islamabad mwezi Julai mwaka huu. Pia shambulizi hilo linakuja siku chache tu kabla rais Pervez Musharraf kugombea tena wadhifa wa urais, licha ya upinzani mkubwa kuhusiana na nyadhifa mbili alizonazo za rais pamoja na kuwa mkuu wa jeshi. Kutokana na hatua ya kupambana na waandamanaji siku ya Jumamosi, ambapo polisi waliwapiga wanasheria na waandishi wa habari nje ya tume ya uchaguzi, serikali ya Pakistan imewasimamisha kazi viongozi wawili wa polisi mjini Islamabad pamoja na afisa wa jiji hilo. Kusimamishwa huko kuliamuriwa na mkuu wa mahakama kuu Iftikhar Muhammed Chaudhry.