Ireland yalaza shingo | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ireland yalaza shingo

Baada ya kujizungusha huku na kule, ikikwepa kujiingiza kwenye deni kama la nchi nyengine za Ulaya, hatimaye Ireland imelazimika kuomba msaada wa kifedha kutoka EU na Kimataifa. Kwa nini nchi hii imemeza matapishi yake?

Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dublin, Jumapili, Nov. 21, 2010. (Picha ya AP/Peter Morrison)

Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dublin, Jumapili, Nov. 21, 2010. (Picha ya AP/Peter Morrison)

Jana (21 Novemba 2010) Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen, alitangaza kile ambacho kilitarajiwa na wachambuzi wengi wa masuala ya fedha, lakini ambacho kilikuwa kinakanwa na serikali yake.

"Nathibitisha kwamba leo hii serikali imeamua kuomba msaada wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya. Ombi hilo limewasilishwa jioni hii na Umoja wa Ulaya umekubalina nalo." Alisema Cowen.

Baada ya wiki kadhaa za sitaki-nataka, hatimaye watu wa Ireland wamepaswa kusahau kiburi chao na kukubaliana na ukweli kwamba, bila ya fedha kwenye makasha ya benki zao, mkate utakosekana mezani. Sasa watachukua msaada wa fedha kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), licha ya masharti yake kuwa mazito, makubwa na magumu.

Hii inakuwa ni nchi ya pili ya Ulaya kujikuta ikilazimika kuomba msaada huu wa kifedha, ikitanguliwa na Ugiriki, ambako hadi sasa hali ya kisiasa haijawa shwari kutokana na wananchi kupingana na msaada huu wanaouona kuwa ni chambo kwenye ndoana.

Lakini, Ireland nayo ilishafikia kwenye mkwamo wa kifedha na sasa ilikuwa lazima ikwamuliwe, vyenginevyo uchumi wake ungelisambaratika vibaya na hivyo kusababisha matatizo sio ya kiuchumi tu, bali ya kisiasa na kijamii. Kama anavyosema, Waziri Mkuu Cowen, watu wa Ireland wanapaswa kujifunza kuishi na ukweli huu, na sasa lazima wajiamini "ili tuweze kupoza majeraha haya na hatimaye tunyanyuke tena."

Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen (kushoto) na Waziri wake wa Fedha Brian Lenihan (kulia) wakijibu masuali ya waandishi wa habari kuhusu nchi yao kukubali msaada wa kifedha kutoka EU na IMF, mjini Dublin, Jumapili, Nov. 21, 2010. (Picha ya EPA/STRINGER)

Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen (kushoto) na Waziri wake wa Fedha Brian Lenihan (kulia) wakijibu masuali ya waandishi wa habari kuhusu nchi yao kukubali msaada wa kifedha kutoka EU na IMF, mjini Dublin, Jumapili, Nov. 21, 2010. (Picha ya EPA/STRINGER)

Waziri wake Fedha, Brian Lenihan, anasema kwamba EU na IMF zimeshauona mkakati wa nchi yake wa miaka minne ya kufunga mkaja, na hatarajii kwamba taasisi hizo zitahitaji kuufanyia marekebisho mpango huo.

Lenihan aliliambia shirika la habari la nchi hiyo, RTE, kwamba kiwango cha kati ya Euro bilioni 80 hadi 90 kitakachoingizwa na Umoja wa Ulaya katika uchumi wa Ireland, kitairuhusu Dublin kurudi haraka kwenye udhibiti wa soko lake, akipingana na hoja ya kiongozi wa Upinzani, Michael Noonan, ambaye amesema kwamba Ireland itajikuta nje ya soko ndani ya miaka mitatu tu ijayo.

Lakini kufa kufaana, kwani kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, leo hii (22 Novemba 2010) thamani za hisa katika masoko barani Ulaya imepanda thamani mara tu baada ya Ireland kukubali kupokea msaada wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya na IMF.

Faharisi ya soko la STOXX Europe 600 ilianza kupanda kutoka asilimia 0.77 hadi alama 271.57, sambamba na ongezeko mfano wa hilo katika masoko kadhaa ya hisa kwenye nchi mbalimbali barani Ulaya. Wakati huo huo thamani ya Euro ikaongezeka kwa asilimia 0.2 mbele ya dola ya Marekani, mara tu maafisa wa fedha wa Ireland na Ulaya walipokaribia kufikia tamati ya mazungumzo yao ya jana (21 Novemba 2010).

Inatarajiwa kwamba, kwa kukubali Ireland kupokea msaada huu wa kifedha, soko la hisa katika mji wa kifedha wa Ulaya, Frankfurt, litafikia alama 7000, ambazo ni za juu kabisa kwa mwaka huu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/REUTERS/DPA

Mhariri: Othman Miraj

DW inapendekeza

 • Tarehe 22.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QF69
 • Tarehe 22.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QF69

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com