1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yaadhimisha mwaka mmoja leo huku hofu ikizidi kutanda nchini humo

21 Desemba 2011

Serikali ya Iraq imeadhimisha mwaka wake wa kwanza hii leo katika hali ya hofu kubwa huku waziri mkuu Nuri Al Maliki akitaka akabidhiwe makamu wa rais wa madhehebu ya Kisunni ili ajibu mashtaka ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/13XFb
Waziri mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki akiwa mjini Washington
Waziri mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki akiwa mjini WashingtonPicha: AP

Serikali ya Marekani imeomba kuwepo utulivu, lakini waziri mkuu Nuri Al Maliki ametishia kuwapiga kalamu mawaziri wote wanaoungwa mkono na kundi la Kisunni la Iraqiya, ikiwa hawatasitisha mgomo wao wa kuhudhuria vikao vya baraza la mawaziri, huku naye makamu wa rais Tareq al Hashemi, ambaye kwa sasa amejificha katika eneo lililojitenga la Kikurdi akikanusha madai kuwa analiongoza genge lililosababisha mauaji.

Wabunge pia wanatarajiwa kutathmini wito wa Maliki wa kumpiga kalamu naibu waziri mkuu Saleh al Mutlak wa madhehebu ya Wasunni, ambaye amelalamikia uongozi wa serikali ya Kishia ya umoja wa kitaifa na kuitaja kuwa ya udikteta.

Haya yote yanajiri siku chache tu baada ya wanajeshi wa Marekani kukamilisha mpango wao wa kuondoka kabisa nchini humo na kuwacha nyuma kile rais Barrack Obama alikitaja kuwa “Iraq iliyo huru, imara na yenye kujitegemea”.

Hashemi alikanusha mashtaka yote dhidi yake na kuapa kupambana mahakamani. Maafisa walitoa waranti wa kukamatwa Hashemi siku ya jumatatu, baada ya kumpiga marufuku  kusafiri katika mataifa ya kigeni.

Makamú wa rais wa Iraq Tariq al-Hashemi anayekabiliwa na madai ya ugaidi
Makamú wa rais wa Iraq Tariq al-Hashemi anayekabiliwa na madai ya ugaidiPicha: dapd

Matamshi ya Maliki yalijiri baada ya yeye kufanya mazungumzo ya simu na makamu wa rais wa Marekani Joe Biden, ambaye alimwomba kushirikiana na vyama vingine ili kutatua mzozo huo unaozidi kutokota na ambao unatishia hali tete ya kisiasa nchini Iraq. Maliki pia alikataa miito ya Hashemi ya wawakilishi wa jumuiya ya Kiarabu kuchunguza upelelezi wote pamoja na maswali yoyote, akiwaambia wanahabari kuwa walimpa dikteta wa Iraq Saddam Hussein hukumu ya haki na watahakikisha kuwa hukumu ya haki pia itatolewa kwa Hashemi.

Kwa upande mwengine Wabunge wanatarajiwa kuamua kuhusu ombi la Maliki la kutimuliwa ofisini Mutlak Januari 3.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed