Iraq ichukue jukumu yenyewe | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iraq ichukue jukumu yenyewe

Leo ni siku ya pili ya ziara ya waziri ya ulinzi wa Marekani, Robert Gates, nchini Iraq. Wakati huo huo, kamanda mmoja wa jeshi la Marekani alisema anataraji kundi la Al-Qaida kuendelea kuishambulia Iraq. Na nchini Marekani, seneta maarufu aliarifu Marekani imeshindwa katika vita hivi vya Iraq.

Baada ya mashambulio mjini Bagdad

Baada ya mashambulio mjini Bagdad

Tangu leo asubuhi, habari juu ya mauaji inaendelea kusikika kutoka Iraq Mwanajeshi mmoja wa Marekani ameuawa katika shambulio dhidi ya kituo cha jeshi la Marekani karibu na Baghdad. Katikati ya Bagdad mtu mmoja alipiga risasa barabarani na kuwaua watu watatu. Na pia mjini Bagdad maafisa wawili wa polisi waliuawa na jambazi.

Haya yametokea wakati waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, yuko Iraq kwa siku yake ya pili baada ya kuwasili jana na kutembelea majeshi yake. Leo Bw. Gates anatarajiwa kukutana na viongozi wa kisiasa wa Iraq na kuwaomba wazidishe kasi katika mradi wa kuleta maridhiano kati ya Wasuni na Washia. Juzi tu watu wasiopungua mia mbili waliuawa katika mashambulio ya mabomu yaliyowekwa ndani ya magari.

Marekani inaitaka serikali ya Iraq ichukue jukumu la kuhakisha usalama katika nchi mwake. Waziri Gates aliwakumbusha Wairaqi kuwa subira ya Marekani ina mwisho wake. Alisema: “Kusema ukweli, ningependa kuona mambo yanaendelea haraka zaidi. Si kwamba sheria zinaweza kubadilisha hali moja kwa moja lakini uwezo tu wa kuzipitisha unaonyesha kuna nia ya kushirikiana, yaani pande zote za serikali ya Iraq zinaanza kutatua alau baadhi ya matatizo yaliyopo.”

Kulingana na meja jenerali Michael Barbero wa jeshi la Marekani, kundi la kigaidi la Al-Qaida limechukua dhamana ya shambulio dhidi ya bunge la Bagdad lililotokea wiki iliyopita, vilevile kundi hili linaaminika lilifanya mashambulio mengine ya hivi karibuni. Meja Barbero alisema inabidi kuitambua hali halisi na kwamba mashambulio ya hali ya juu yataendelea.

Wakati huo huo, seneta maarufu wa chama cha Demokratik cha Marekani, Harry Reid, alitangaza Marekani imeshindwa nchini Iraq. Reid aliikosoa hatua ya kupelekwa wanajeshi zaidi ikiwa ni mkakati mpya wa rais Bush. Reid alisema: “Mpango huo haukuleta mafanikio yoyote kama inavyoonekana kutokana na mashambulio mabaya yaliyotokea Iraq wiki hii.” Chama cha Demokratic chenye wingi katika bunge na serikali ya rais Bush wanagombana juu ya fedha za kugharamia hatua hiyo ya dharura. Wademokratik wanataka kuwekwa tarehe ya kuondosha majeshi kutoka Iraq, lakini rais Bush alisema atakataza hilo kwa kupiga kura ya turufu.

Katika mkutano na waandishi wa habari, seneta Reid alimkumbusha rais Bush juu ya vita vya Vietnam ambapo pia rais wa zamani aliongeza idadi ya wanajeshi licha ya kujua kwamba hakuna ushindi wa vita hivyo. Reid alisem, kushinda vita vya Iraq ni kwa njia ya kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi tu, lazima rais ayatambua haya. Rais Bush lakini, alipoulizwa juu ya mfano wa Vietnam alisema huko mamillioni ya watu walikufa baada ya Wamarekani kuondoka. Ndiyo sababu anahofu kwamba haya yanaweza kutokea pia nchini Iraq, alisema Bush.

 • Tarehe 20.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHFo
 • Tarehe 20.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHFo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com