Iran yazionya nchi za magharibi juu ya kutumia nguvu dhidi yake | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 17.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Iran yazionya nchi za magharibi juu ya kutumia nguvu dhidi yake

Onyo hilo limetolewa leo baada ya waziri wa mambo ya nje kusema kuna uwezekano wa kuvamiwa Kijeshi Iran ikiwa itaendelea kukaidi mapendekezo ya baraza la Usalama la UN

''Mpango wa Nuklia wa Iran umekuwa ukitiliwa shaka na nchi za Ulaya na Marekani''

''Mpango wa Nuklia wa Iran umekuwa ukitiliwa shaka na nchi za Ulaya na Marekani''

Onyo la Iran limetolewa siku moja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa kutishia juu ya kuivamia Iran kufuatia mpango wake wa Kinuklia hatua ambayo sasa imeungwa mkono pia na Ujerumani,Uholanzi na mataifa mengine ya Ulaya.

Makamu war ais wa Iran Reza Aghazadeh akizungumza mbele ya mkutano mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti technologia ya Nuklia IAEA mjini Vienna amesema nchi za Magharibi siku zote zimekuwa zikichagua njia ya kutumia nguvu badala ya kutafuta maelewano na mahusiano mazuri kuelekea taifa la kiislamu la Iran.

Matamshi hayo ya Iran yametolewa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner kuonya hapo jana kwamba ulimwengu unapaswa kukubali uwezekano wa kutumiwa nguvu dhidi ya Iran endapo taifa hilo litazidi kuwa kaidi katika mzozo wa Kinuklia.

Akiulizwa ana maana gani Bw Kouchner alijibu „ Ninamaana ya Vita mshehimiwa“ na akaendelea kusema kuwa ;-

``Tunajitayarisha, tukijaribu kwanza kuandaa mpango kupitia wakuu wa majeshi, na hilo si jambo la kesho. Tunajiandaa kutukisema hatukubali kingine zaidi ya kusitishwa urutubishaji wa Uranium. Mpaka sasa hakuna kinachofanyika hivyo tunapendekeza vikwazo vikali zaidi hatimae vitekelezwe’’.

Vyombo vya habari vya Iran vimeishutumu Ufaransa kwa kujitwika sera za Marekani juu ya mgogoro huu huku makamu war ais wa Iran ambaye pia anaongoza shirika linalohusika na masuala ya nishati ya Atomiki nchini Iran akiyakosoa baadhi ya mataifa ya Magharibi ambayo yamejionyesha hayawezi kukubali mataifa mengine huru na yanayoendelea kujitafutia technologia ya kisasa.

Aidha amesema Iran imeshagundua tabia hiyo ya kibaguzi na ikiwa mataifa hayo ya kimagharibi yatachukua njia ya ushirikiano bila shaka changamoto katika uwanja wa kimataifa inaweza kuzuilika.

Lakini amesisitiza pia kwamba inachokitaka Iran ni kuwa na Nuklia kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya umeme na kwahivyo itaendelea na shughuli za mradi wake wa Nuklia ambao mataifa ya Magharibi yanasema unanuiwa kutengenezea silaha za Nuklia.

Akiufungua mkutano wa Vienna mkuu wa shirika la Kimataifa la kudhibiti technologia ya Nuklia IAEA Mohammed El Baradei alisema inasikitisha sana kwamba Iran imekataa kuzingatia mapendekezo ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa yanayoitaka Iran isimamishe shughuli za kurutubisha madini ya Uranium ambayo yanaweza kutumika katika utengenezaji wa mabomu.

Lakini Sio Tu Ufaransa inayotaka Iran ivamiwe kijeshi Ujerumano nayo inashirikiana kwa karibu na Ufaransa na washirika wengine kukikabili kitisho cha Iran.Msemaji wa serikali ya Ujerumani Ulrich Wilhelm amesema Ufaransa haijakosea hata kidogo kwamba umewadia wakati wakufanyika kila kinachowezekano kuhakikisha Iran haliwi taifa lenye silaha za Nuklia.Lakini waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Martin Jaeger kwa upande wake amesema hajayachukulia matamshi ya Kouchner kuwa ni kitisho cha vita ila Ufansa na Ujerumani zinashirikiana juu ya duru ya tatu ya vikwazo dhidi ya Iran.Uholanzi nayo imesema inaunga mkono vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran ikiwa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa litashindwa kukubaliana kuhusu hatua nyingine ya kuchukuliwa dhidi ya Iran.

 • Tarehe 17.09.2007
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB1A
 • Tarehe 17.09.2007
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB1A

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com