1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatuhumiwa kula njama kumuua balozi wa Saudia Marekani

Saumu Ramadhani Yusuf12 Oktoba 2011

Marekani na Iran katika mvutano juu ya tuhuma za jaribio la kumuua balozi wa Saudia,Washington

https://p.dw.com/p/12qZK
Mwanasheria mkuu wa Marekani Eric HolderPicha: dapd

Spika wa bunge la Iran amekanusha madai yaliyotolewa na Marekani ya kuituhumu nchi yake kwamba imehusika kupanga njama ya kumuua balozi wa Saudi Arabia mjini Washington. Iran inasema madai hayo ni mchezo wa kitoto unaokusudiwa kuyavuruga mawazo ya wamarekani. Maafisa wa Marekani jana walisema wamegundua njama ya watu wawili wanaohusishwa na mashirika ya kiusalama ya Iran ya kutaka kumuua balozi Adel al Jubeir. Rais Obama ameitaja njama hiyo kama ni kitendo cha dhahiri kinachokiuka sheria za Marekani na za Kimataifa.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, amesema anataraji kwamba nchi zinazosita kuiwekea vikwazo Iran sasa zitabadili mitazamo yao baada ya tukio hilo.

NO FLASH Saudi-arabischer US-Botschafter Adel al-Jubeir
Balozi wa Saudi Arabia nchini MarekaniPicha: dapd

Waziri wa sheria wa Marekani, Eric Holder, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habar mjini Washington hapo jana alisema ni tukio lililokuwa kama la kijaasusi. Njama hiyo ilikuwa ni ya kumuua balozi wa Saudi arabia mjini Washington katika jaribio la kumshambulia kwenye mkahawa mmoja katika mji mkuu huo wa Marekani. Hata hivyo, njama hiyo ya watu wawili iligunduliwa kabla haijafanyika. Mmoja kati ya watuhumiwa hao ni mwanamme mwenye umri wa miaka 56 mwenye uraia wa Marekani na pia anayeshikilia hati ya usafiri ya Iran na ambaye alikamatwa mwezi wa Septemba mjini New York na kutiwa ndani. Mwingine anasadikiwa kuwa huru huko nchini Iran, akitumikia jeshi la kimapinduzi nchini humo.Mwanasheria mkuu wa Marekani amesema ni wazi kwamba Iran inahusika moja kwa moja na njama hiyo.Waziri huyo amesema kwamba,

''Marekani inabaini kuibebesha dhamana Iran kwa vitendo vyake.''

Kugunduliwa njama hiyo kumetokana na hatua inayohusisha usikilizaji wa simu za kimataifa, na ufuatiliaji wa fedha zinazotokana na mihadarati kutoka Mexico. Mfanyikazi mmoja wa shirika la Marekani la kupambana na mihadarati ndiye aliyewagundua wauwaji. Holder akifafanua zaidi amesema mfanyikazi huyo mwezi Mei alijitolea kujiunga na wafanyibiashara wa madawa ya kulevya huko Mexico wanaosakwa na alikutana nao mara kadhaa. Juu ya hayo alipewa kazi ya kumuua balozi huyo wa Saudi Arabia Adel al Jubeir kwa malipo ya dolla milioni 1.5. na tayari malipo ya mwanzo ya dolla 100,000 alishawekewa katika akaunti yake ya kibinafsi.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa tahadhari ya miezi mitatu kote duniani kwa raia wake ikionya kwamba kuna mipango ya kushambuliwa wamarekani, wakiwemo ndani ya Marekani. Aidha maafisa wa Marekani wanasema kwamba kumekuweko mijadala kuhusu njama nyinginezo zinazodaiwa kupangwa na Iran, ikiwemo kuzishambulia ofisi za balozi za Saudi Arabia na Israel mjini Washington. Hata hivyo, madai hayo hayakutajwa hapo jana. Balozi wa Iran nchini Marekani amezipinga kauli za tuhuma dhidi ya nchi yake, akimuandikia barua katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akisema Marekani ina njama ya kuipaka matope Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mwandishi Paulert Rüdiger/Saumu Mwasimba/ZR

Mhariri: Miraji Othman