1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iran yafanya uchaguzi wa ubunge kwa utulivu

Wairan wanachagua wabunge leo (02.02.2012); uchaguzi unaoonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa zoezi la uchaguzi wa urais mwakani. Suala la uchumi linapewa kipaumbele na wapiga kura hao wameombwa kujitokeza kwa wingi.

Raia wakipiga kura ya ubunge leo (02.03.2012)

Raia wakipiga kura ya ubunge leo (02.03.2012)

Zoezi hilo la uchaguzi wa wabunge linalofanywa leo linatarajiwa kuimarisha nguvu ya kiongozi mkuu wa kidini, Ayatollah Ali Khamenei, dhidi ya wapinzani wa kisiasa wenye msimamo mkali, wanaoongozwa na Rais Mahmoud Ahmadinejad.

Hata hivyo, kura hiyo haionekani kuwa na athari kubwa kwa sera za nje za Iran wala kwa mpango wake tata wa nyuklia, na tayari uhusiano wa kidiplomasia na mataifa ya nje unadhibitiwa vikali na Khamenei.

Lakini, matokeo ya uchaguzi huu yanaweza kumruhusu kiongozi huyo wa kidini, kuimarisha maamuzi yake kwa mustakabali wa siasa za Iran, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa urais mwakani.

Rais wa Iran Mahmud Ahmadined akitoa hotuba

Rais wa Iran Mahmud Ahmadined akitoa hotuba

Huku Iran ikitengwa na kukabiliwa na vikwazo kutoka nchi za Magharibi, kufuatia mpango wake wa nyuklia na kitisho cha kushambuliwa na Israel, viongozi wa Iran wametoa wito kwa raia wao kupiga kura kwa wingi ili kuunga mkono uhalali wa utawala wao.

Mara tu baada ya kupiga kura yake, Khamenei amesema kuna propaganda nyingi hasi dhidi ya taifa hilo, huku mataifa yenye nguvu na yenye kujigamba yakiwalazimisha kufanya yanachotaka. Khamenei aidha amesema jambo la msingi ni raia kujitokeza kwa wingi kwa manufaa na usalama wa Iran.

Hassan Hashemiyan ni mtaalam wa masuala ya jamii kutoka Chama cha Farsi. "Katika duru hii ya uchaguzi, bila shaka ushindani upo katika chama kimoja pekee. Kwa sababu makundi mengine ya kisiasa kama vile Wanamapinduzi, Waliberali na Wafuasi wa siasa za mrengo wa shoto, hayapo tena. Kwa hiyo, kinyang'anyiro kilichopo sasa ni miongoni mwa chama kimoja tu cha siasa," amesema Hassan.

Ishara ya nyuklia katika Bendera ya Iran

Ishara ya nyuklia katika Bendera ya Iran

Uchaguzi huu wa leo ni wa kwanza tangu mwaka 2009, wakati uchaguzi wa urais ulipopingwa na maandamano ya wapinzani na wanaharakati wa demokrasia yalipozimwa na vikosi vya Jeshi la Serikali.

Mwaka huu, makundi yenye nguvu ya wanamapinduzi yamesema yatakaa pembeni, na kutoa mwanya wa upinzani mkali baina ya wafuasi wa kiongozi wa kidini, Khamenei na Rais Ahmadinejad.

Vyama viwili vinavyoshindania viti 290 vya ubunge ni United Front of Principlists, kinachomuunga mkono Khamenei na Resistance Front chenye wafuasi wengi wa Rais Mahmoud Ahmadinejad.

Mwandishi: Pendo Paul\ Reuters

Mhariri: Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com