1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yatauma waraka kwa Facebook

29 Machi 2018

Serikali ya India imetuma waraka  kwa Facebook ikitaka kujua iwapo kampuni ya Uingereza ya Cambridge Analytica ilitumia data za wapigaji kura wa taifa hilo na watumiaji wa Facebook kuwashawishi kwenye uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/2vDha
Symbolbild Facebook und Indien
Picha: picture-alliance/NurPhoto/N. Kachroo

 

Waraka mwengine kama huo ulitumwa juma lililopita kwa kampuni ya Cambridge Analytica baada ya taarifa kwenye vyombo vya habari kudai kwamba, ilitumia data za raia wa India na kuathiri matokeo ya uchaguzi.

Serikali ya India imeweka tarehe 7 Aprili kuwa mwisho wa kampuni ya Cambridge Analytica kujibu waraka wake.

Facebook inakabiliwa na tuhuma baada ya ripoti kwamba kampuni hiyo ya Uingereza ilipata data ya mamilioni ya watu kwa njia haramu kutoka kwa watumiaji wa Facebook ili kuathiri matokeo ya uchaguzi.

India yataka Facebook kujibu ifikapo tarehe 7, Aprili

Kwenye taarifa yake siku ya Jumatano, Wizara ya Habari, Elektroniki na Teknolojia nchini India ilisema kuwa Facebook ina watumiaji wengi nchini humo na ilitaka kujua iwapo, ni hatua zipi inazochukua kuhakikisha usalama na siri ya watumiaji wake wengi ili data zao zisiweze kutumiwa vibaya na mtu mwengine.

Chama tawala cha Bharatiya Janata na kile cha upinzani vimeshutumiana kwa kutumia huduma za kampuni hiyo ya Uingereza lakini vikakanusha uhusiano wowote nayo.

Fünf Möglichkeiten, ausgetrocknete Städte cooler zu machen
Afisi za Cambridge Analytica, UingerezaPicha: Reuters/H. Nicolls

Inadaiwa kuwa kampuni ya Cambridge Analytica ilitumia bila ya ruhusa data za watumiaji wa Facebook zinazohusiana na data kwenye mashine za kupigia kura, suala ambalo limeibua mjadala kuhusu faragha kwenye matumizi ya vyombo vya kidijitali.

Wataalamu wa masuala ya dijitali wanasema sheria za udhibiti nchini humo zina mapungufu makubwa.

Waraka wa serikali ya India ulitaka kujua, "iwapo Facebook imewahi kuhusika kuathiri mchakato wowote wa uchaguzi nchini humo."

Wakati huo huo, Facebook siku ya Jumatano ilizindua mkakati mpya wa kuzima madai dhidi yake ya kudukua data za watu binafsi, kwa kuweka kitufe cha kibinafsi ambacho kitamuwezesha mtumiaji kuwa na udhibiti mkubwa wa habari au maelezo yake.

Mkakati huo mpya unajiri baada ya mtandao huo mkubwa wa kijamii kukosolewa baada ya kufichuliwa kuwa data za mamilioni ya watumiaji wake zilitumiwa na kampuni ya Uingereza inayohusishwa na kampeini za rais wa Marekani Donald Trump mwaka 2016.

Kampuni ya Facebook imekiri kuwa inahitaji kufanya mengi ili kuwafahamisha watu lakini imesema kuwa mabadiliko yako njiani.

Afisa mkuu wa masuala ya faragha wa kampuni hiyo Erin Egan na naibu mwanasheria wake, Ashlie Beringer, wamesema hayo kwenye taarifa ya blogu.

"Tunachukua hatua za ziada katika wiki zijazo kuzidisha faragha ya watumiaji."

Facebook yaweka mikakati mipya ya kuboresha utumiaji

Mikakati hiyo mipya inajumuisha upatikanaji wa haraka na njia rahisi ya mpangilio wa vitufe vya kutafuta, kupakua na pia kufuta data za mtu binafsi katika mtandao huo unaotumiwa na takriban watu bilioni mbili.

Facebook imesema kuwa menyu mpya itawawezesha watumiaji kuboresha usalama wa akaunti zao na kudhibiti matangazo pindi wayaonapo.

Mark Zuckerberg als Student 2004
Mark Zuckerberg mmoja wa waanzilishi wa FacebookPicha: picture-alliance/Photoshot

Sera ya sheria na masharti ya Facebook yanarekebishwa kuboresha uwazi wa jinsi inavyokusanya habari za watumiaji kwa mujibu wa Beringer na Egan.

Mtandao huo wa kijamii umesema pia unafunga kabisa kitengo ambacho hutumiwa sana na wanaobandika matangazo yao.

Mapema mwezi huu, mfichuasiri Christopher Wylie alifichua kuwa kampuni ya kutoa ushauri ya Cambridge Analytica ilipata habari za watumiaji milioni 50 wa Facebook kupitia utafiti wa kiakademia.

Pamoja na hayo wachambuzi wengine wanasema kuwa Facebook na mkuu wake Mark Zuckerberg wametoa ahadi kama hizo siku za nyuma.

Wachambuzi wasifia hatua ya Facebook

Profesa Zeynep Tufekci wa Chuo Kikuu cha North Carolina, kwenye mtandao wake wa titwa alisema, "Zuck aliahidi udhibiti mzuri wa siri katika wiki zijazo, miaka minane iliyopita."

Profesa Jennifer Grygiel wa Chuo Kikuu cha Syracuse alisema, "mkakati mpya ni mzuri sana, nashangaa kwa nini hatua hiyo haikuchukuliwa mapema."

Christopher Wylie
Christopher Wylie mfichua siri wa sakata ya Cambridge AnalyticaPicha: picture-alliance/dpa/Uncredited/PA

Dylan Gilbert wa kampuni ya Public Knowledge amesema kuwa, "hatua ya Facebook ni nzuri na inakaribishwa na kila mmoja, lakini sio suluhisho kwa matatizo makubwa."

Halmashauri ya Biashara ya Shirikisho la Marekani, juma hili ilizindua uchunguzi wa iwapo Facebook ilikiuka sheria za ulinzi za wateja ama maafikiano ya mahakama mwaka 2011 ya kulinda matumizi ya data za kibinafsi.

Wabunge wa Marekani wanajaribu kumpata Zuckerberg aje Washington kutoa ushahidi kuhusu suala hilo.

Mamlaka nchini Uingereza zimetwaa data za kampuni ya Cambridge Analytica huku Umoja wa Ulaya ukionya kuwepo kwa athari kwa Facebook.

Mwandishi; Shisia Wasilwa, Reuters 

Mhariri: Saumu Yusuf