Idadi ya wakaazi duniani imefikia watu bilioni saba | Masuala ya Jamii | DW | 31.10.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Idadi ya wakaazi duniani imefikia watu bilioni saba

Katibu mkuu Ban Ki Moon amesema mtoto atakayetimiza idadi hii atakuwa katika dunia inayokabiliwa na utata, na changamoto kubwa katika vita dhidi ya umasikini.

Newly born babies lie at a government hospital in Hyderabad, India, Monday, Oct. 31, 2011. According to the U.N. Population Fund, there will be a symbolic seven billionth baby sharing Earth's land and resources on Oct. 31. Already the second most populous country with 1.2 billion people, India is expected to overtake China around 2030 when its population soars to an estimated 1.6 billion. (Foto:Mahesh Kumar A./AP/dapd)

Umoja wa mataifa washerehekea idadi ya wakaazi kuwa bilioni saba

Ban Ki Moon amesema ingawa kutakuwa na vigelegele vya kuwakaribisha watoto wachanga, tukio la dunia kufikisha wakazi bilioni saba halipaswi kuchukuliwa kimzaha.

Ingawa nchi tofauti ulimwenguni zimetangaza kuwa mahali alikozaliwa mtoto aliyeifanya idadi ya wakazi wa dunia kufikia bilioni saba leo, katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon hatafanya ishara ya kumpakata yeyote miongoni mwa watoto hao, kama alivyofanya mtangulizi wake Kofi Annan huko Sarajevo, tarehe 12 Oktoba mwaka 1999, dunia ilipofikisha watu bilioni 6. Katibu mkuu huyo wa umoja wa mataifa, amesema dunia kufikisha wakazi bilioni saba si suala la kuchukuliwa kimzaha.

Katika mahojiano na gazeti la Time Magazine, Ban Ki Moon amesema dunia yenye idadi kama hiyo ni dunia inayokabiliwa na mapambano makali dhidi ya umasikini. Alisema na hapa namnukuu; '' Kuna chakula tele duniani, lakini bado watu bilioni moja wanalala njaa kila siku, watu wengi wanaishi maisha ya anasa, lakini wakati huo huo kwa watu wengine umasikini unazidi kuongezeka. Kuzaliwa kwa mtoto wa bilioni saba kunapaswa kuwa kama mbiu ya kuiamsha dunia kuchukua hatua.'' Mwisho wa kumnukuu.

Ban Ki Moon kandidiert für zweite Amtszeit Flash-Galerie

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon

Takwimu kuambatana na tukio la leo zinaonyesha idadi ya watu inaongezeka kwa kasi kubwa katika nchi masikini ikilinganishwa na mataifa yenye uchumi uliostawi, na kwa mantiki hiyo umoja wa mataifa umetoa wito kwa nchi tajiri kutoa kuelekeza misaada zaidi kwenye kampeni ya uzazi wa mpango.

Lakini, kama alivyosisitiza katibu mkuu wa umoja wa mataifa, idadi ya watu bilioni saba wanaoishi duniani sasa haipaswi kuchukuliwa kama tukio la kitakwimu tu. Inapaswa kuchukuliwa pia kama idadi ya watu wanaohitaji chakula cha kutosha na nishati katika maisha yao. Watu wanaohitaji kupata elimu kama nyenzo ya kuboresha maisha yao, wanaohitaji kuishi kwa uhuru na heshima, na matumaini ya wao pia kupata haki ya kuzaa watoto na kuwalea katika mazingira salama. Kila kitu ambacho unakihitaji kama binadamu, alisema Ban Ki Moon, sasa zidisha mara bilioni saba!

Ujumbe huu Bwana Ban Ki Moon anatarajiwa kuufikisha kwenye mkutano wa viongozi wa nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, ambao utafanyika mjini Paris, Ufaransa wiki hii. Mkutano huo utapaswa kutilia maanani kuwa ongezeko la watu duniani na mgogoro wa kiuchumi unaoendelea kwa pamoja vitazusha mizozo zaidi kama ile inayoendelea katika ulimwengu wa kiarabu, na maandamano yaliyopewa jina la "Occupy Wall Street" huko Marekani.

Wito wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa kuwa sasa ni wakati wa kuchukua hatua, unazitaka nchi za dunia kushirikiana zaidi ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza baadaye wakati idadi kubwa ya watu itakapokuwa ikigombania raslimali zisizoongezeka.

Mwandishi: Daniel Gakuba/Reuters/ AFP

Mhariri:Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com