ICC yaanza kuichunguza Boko Haram | Matukio ya Afrika | DW | 04.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

ICC yaanza kuichunguza Boko Haram

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Fatou Bensouda, ameitaka serikali ya Nigeria kuchunguza uhalifu unaofanywa na kundi la Boko Haram baada ya Mahakama yake kuanza kulifuatilia kundi hilo.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda.

Licha ya kusema kwamba tayari ameshamueleza Rais Jonathan Goodluck kuhusu uchunguzi wa awali wa Boko Haram, Bensouda amesisitiza kwamba mahakama yake haifanyi uchunguzi rasmi wa ghasia zinazotokea kaskazini mwa Nigeria.

"Hali ya Nigeria bado ipo kwenye uchunguzi wa awali tu, na ikiwa kama tutaona kwamba matukio yale yale ya uhalifu ndiyo yanayoshughulikiwa na serikali ya Nigeria, basi hakutakuwa na haja ya ICC kuingilia kati." Bensouda aliwaambia waandishi wa habari mjini Abuja.

Bensouda amesema kwamba si lengo la Mahakama yake kuingilia mambo ya ndani ya Nigeria, licha ya kwamba matukio ya kigaidi yanayotokea yanaweza pia kufanana na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Rais Jonathan ataka mazungumzo na Boko Haram

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.

Mwanasheria huyo wa ngazi ya juu wa ICC, amesema kwamba Nigeria yenyewe ina jukumu la kimsingi la kufanya uchunguzi wa kadhia hiyo ya Boko Haram. Kundi hilo limedai kuhusika na mashambulizi yaliyowaua zaidi ya watu 1,000 tangu katikati ya mwaka 2009 na ghasia zimeongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Kufuatia mashambulizi mabaya kabisa ambayo yalisababisha vifo vya watu 185 katika mji wa Kano hapo Januari 20, Rais Jonathan aliwataka Boko Haram kuingia kwenye mazungumzo. Lakini rais huyo amemwambia Mwendesha Mashtaka wa ICC kuwa serikali yake haitatoa kinga ya kutoshitakiwa kwa makosa makubwa ya uhalifu.

Kwa miaka kadhaa pia, ICC imekuwa ikichunguza ghasia za kidini nchini Nigeria katika kile kinachoitwa "Mkanda wa Kati", ambao unaigawa jamii ya kusini yenye Wakristo wengi na ya kaskazini yenye Waislamu wengi.

"ICC si kwa Waafrika tu"

Mmoja wa viongozi wa Afrika aliyefikishwa ICC, Jean-Pierre Bemba wa DRC.

Mmoja wa viongozi wa Afrika aliyefikishwa ICC, Jean-Pierre Bemba wa DRC.

Bensouda, mwanasheria wa Gambia, alianza kazi ya mwendesha mashtaka mkuu wa ICC katikati ya mwezi uliopita, akichukua nafasi ya Luis-Moreno Ocampo, raia wa Argentina, anayekosolewa na baadhi ya viongozi wa Kiafrika kwa kile walichokiita tabia ya mahakama hiyo kuangazia migogoro ya Afrika peke yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais Jonathan, Bensouda amemwambia Rais huyo kwamba mahakama yake haikuwa imeilenga Afrika tu, lakini uchunguzi wake katika uhalifu wa kivita uliofanywa kwenye bara hilo, ulikuwa ni kwa maslahi ya Waafrika walioathirika.

Hadi sasa ICC imeshafungua kesi katika mataifa ya Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan, Kenya, Libya na Cote d'Ivoire, lakini pia imeanzisha uchunguzi wa awali kwa mataifa ya Afghanistan, Colombia, Georgia, Honduras, Guinea na mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na vikosi vya Korea ya Kaskazini dhidi ya raia wa Korea ya Kusini.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman