1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huyu hapa ndiye Muammar Gaddafi

20 Oktoba 2011

Alikuwa mtoto wa wafugaji wa Kibedui, mwenye maisha ya utata, lakini ambaye alitukuzwa sana hadi kufikia kumfananisha na Mtume Mohammad, huku mataifa ya Kimagharibi yakimuona mtu wa hatari wakati wote.

https://p.dw.com/p/12w5U
Muammar Gaddafi katika uhai wake
Muammar Gaddafi katika uhai wakePicha: dapd

Muammar Muhammad Gaddafi aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40. Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake.

Lakini wakati huo, tayari Gaddafi alikuwa ameshatumia njia za kikatili kuyazima maandamano dhidi yake, maandamano ambayo baadaye yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa, watu zaidi ya 30,000 waliuawa kwenye vita hivyo. Mara nyingi sana, Gaddafi alitoa matamko makali wakati wa vita hivyo, ila linalojuilikana zaidi ni lile la kuwaita wapinzani wake kuwa ni panya.

Kwa kila hali, yaliyotokea ni mambo ambayo Gaddafi hakuyatarajia asilani. Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss hapo mwaka 1969.

Muammar Gaddafi akiwa na viongozi mbalimbali duniani
Muammar Gaddafi akiwa na viongozi mbalimbali dunianiPicha: picture-alliance/dpa

Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani.

Anaweza kuchukiwa kwa mengi, lakini ukweli lazima usemwe kwamba huyu ni kiongozi aliyesimama imara kupinga ukoloni wa aina yoyote na wala asiyeogopa kusema lolote dhidi ya wakoloni.

Gaddafi aliwahi kuwaambia watu wake kuwa viungo vinavyotengeneza Coca Cola na Pespi vinatoka Afrika, kwa hivyo Waafrika walipaswa kutengeneza soda hizo wenyewe. Aliupa msukumo mkubwa Umoja wa afrika kwa hali na mali. Akijiita Mfalme wa Wafalme wa Afrika, Gaddafi alitoa mabilioni ya fedha kuendeleza miundombinu ya utalii katika mataifa rafiki.

Lakini katika medani ya kimataifa, jina lake liliingia doa kubwa baada ya kubainika kuwa alikuwa akitoa mafunzo kwa makundi ya kigaidi, likiwemo la RAF la Ujerumani na IRA la Ireland ya Kaskazini. Alishukiwa pia kuhusika na mashambulizi katika klabu ya burudani jijini Berlin. Aliwahi pia kuwa pia muungaji mkono wa waasi wa Chad na Ghana.

Kubwa katika yote, ni mashambulizi dhidi ya ndege ya abiria ya Shirika la Pan Am katika anga ya Lockerbie, Scotland. Kwa hili, dunia haitamsahau daima.

Mwandishi: Hans Michael Ehl/ZPR
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Josephat Charo