Hukumu ya Khodorkovsky | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hukumu ya Khodorkovsky

Ujerumani, Amnesty International na Umoja wa Ulaya waizungumzia hukumu ya tajiri mkubwa nchini Urusi, Mikhail Khodorkovsky.

default

Mikhail Khodorkovsky.

Serikali ya Ujerumani leo imetoa maelezo ya tahadhari kuhusu hukumu iliyotolewa dhidi ya tajiri mkubwa nchini Urusi, Mikhail Khodorkovsky, ambaye amepatikana na hatia ya matumizi mabaya ya fedha.

Msemaji wa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema kuwa hukumu dhidi ya kesi hiyo ingeweza tu kutolewa mara moja iwapo uamuzi kamili ungekuwa unajulikana, ikiwa ni pamoja na uhalali wa mahakama hiyo kutoa hukumu. Msemaji huyo wa serikali ya Ujerumani, Christoph Steegmans amesema walikuwa wanaifuatilia kesi hiyo kwa ukaribu sana na inaupima mfumo wa mahakama nchini Urusi.

Hata hivyo, awali Kamishna wa Haki za Binaadamu nchini Ujerumani, Markus Loenig aliita hukumu hiyo kama mfano wa haki holela za kisiasa. Loenig amesema kuwa alihudhuria sehemu ya kesi hiyo na kwamba ushahidi uliotolewa haukuendana na tuhuma dhidi ya Khodorkovsky. Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International limetaka uchunguzi huru dhidi ya mashtaka ya Bwana Khodorkovsky ufanyike upya.

Mtaalamu wa masuala ya Urusi wa shirika hilo la Amnesty International, Peter Franck amesema kuwa hukumu hiyo na kesi nzima inaonyesha jinsi gani Urusi ilivyo mbali na utawala wa sheria. Bwana Franck amesema kesi hiyo haikuzingatia haki, upande wa utetezi uliwekewa pingamizi na mashahidi wa mtuhumiwa hawakusikilizwa mahakamani. Mtaalamu huyo wa Amnesty International pia amekosoa jinsi siasa ilivyoingilia kati katika kesi hiyo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton leo amesema kuwa alitarajia kuwa Urusi itaheshimu haki za kimataifa na majukumu ya utawala wa sheria wakati wa kutoa hukumu dhidi ya Bwana Khodorkovsky. Bibi Ashton amesema kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kufuatilia kwa ukaribu kabisa maendeleo ya kesi hiyo, ikiwemo tangazo la hukumu ijayo.

Bibi Ashton, amesema kama ilivyosisitizwa katika mkutano wa Umoja wa Ulaya uliofanyika tarehe 7 mwezi huu wa Desemba mjini Brussels, kwamba umoja huo unatarajia kuwa Urusi itaheshimu majukumu ya kimataifa katika nyanja ya haki za binaadamu na utawala wa sheria. Mahakama Kuu ya Urusi, chini ya Jaji Viktor Danilkin, leo iliwakuta na hatia ya ubadhirifu wa fedha Mikhail Khodorkovsky pamoja na mshitakiwa mwenza Platon Lebedev.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE,AFPE)

Mhariri:Josephat Charo

 • Tarehe 27.12.2010
 • Mwandishi Kabogo, Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zqMH
 • Tarehe 27.12.2010
 • Mwandishi Kabogo, Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zqMH

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com