1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hujuma za magaidi dhidi ya kanisa mjini Baghdad zalaaniwa kote ulimwenguni

Oumilkher Hamidou1 Novemba 2010

Mahabusi na polisi zaidi ya 52 wameuwawa vikosi vya usalama vilipojaribu kuwavunja nguvu magaidi waliolivamia kanisa kuu la mjini Baghdad

https://p.dw.com/p/Pvdr
Vikosi vya usalama vyapiga doria nje ya kanisa la kikatoliki la mjini Baghdad baada ya wanamgambo kuwateka nyara kwa zaidi ya saa nne waumini 120 wa kikristo kabla ya vikosi vya usalama kuingilia katiPicha: AP

Watu wasiopungua 52 wameuwawa na wengine 70 kujeruhiwa pale vikosi vya usalama vilipolivamia kanisa moja kuu la kikatoliki mjini Baghdad ili kuwakomboa waumini zaidi ya mia moja waliotekwa nyara na wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam. Kufuatia mauaji hayo Ujerumani imetaka jamii wa Wakrsito walio wachache nchini Irak ilindwe zaidi.

Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Iraq,jenerali Hussein Kamal amesema idadi hiyo ya waliouwawa si pamoja na waasi .Kundi lijiitalo "Dola ya kiislam ya Iraq" linalojifungamanisha na Al Alqaida limedai kuhusika na kisa cha kuvamiwa kanisa kuu la Sayyidat-al Nadjat kilichopelekea pia watu 67 kujeruhiwa.

Kundi la waasi waliokuwa na silaha walilivamia kanisa hilo kuu la mjini Baghdad ambako umati wa waumini walikuwa wakisikiliza misa na kudai wanaharakati wa kiislam waliofungwa nchini Iraq na Misri waachiwe huru.Mapadri wawili wameuliwa na magaidi hao waliotishia pia kuwauwa waumini 120 waliowateka.

Katika ripoti yao kupitia mitandao ya Internet ya wafuasi wa itikadi kali,kundi hilo la kigaidi limesema linalenga pia kanisa la Koptik la nchini Misri.

Afisa mmoja wa polisi ambae hakutaka jina lake litajwe amesema opereshini ya vikosi vya usalama ilikuwa ya shida kwasababu waasi walijichanganya na umati wa waumini.

Mbunge mmoja wa kikatoliki ameikosoa hatua ya vikosi vya usalama na kusema ukosefu wa serikali,miezi minane baada ya uchaguzi wa bunge,March 7 iliyopita,umeacha mwanya unaotumiwa na waasi.

"Ni jambo linalotia uchungu sana na kusikitisha" amesema kasisi mmoja mjini Baghdad.

"Tumekosa nini.Wanataka tundoke,na serikali inafanya nini.Haifanyi chochote" amesema kwa upande wake askofu mkuu Pios Kasha.

Vatikan Papst Benedikt XVI in Rom
Papa Benedikt wa 16Picha: AP

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,Papa Benedikt wa 16 amelaani vikali hii leo "matumizi ya nguvu yasiyokuwa na maana na ya kikatili dhidi ya watu wasioweza kujihami nchini Iraq.

Papa Benedikt wa 16 ameelezea mshikamano wake pamoja na jamii ya wakristo na kutoa mwito kwa mara nyengine tena wa kupatikana amani. Wakati huo huo Ujerumani imetoa mwito jamii ya Wakristo walio wachache nchini Irak walindwe zaidi. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Stefen Seibert amewaambia waandishi habari mjini Berlin hii leo kuwa Ujerumani imeshtushwa na kusikitishwa na kisa cha kuuliwa waumini katika kanisa.

Viongozi wa opereshini ya Baghdad dhidi ya magaidi wamenukuliwa na kituo cha televisheni wakisema watumishi wawili wa kituo cha televisheni cha Baghdadiya wamekamatwa.Wanatuhumiwa kupokea taarifa ambamo magaidi wameelezea madai yao.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,reuters/dpa

Mpitiaji: Josephat Charo