1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Feri zaharibika Mombasa na kuwakwamisha maelfu ya abiria

Mjahida 26 Oktoba 2015

Maelfu ya wasafiri walikwama katika kivuko cha Feri cha Likoni mjini Mombasa Kenya kufuatia kuharibika kwa feri tatu zinazohudumu katika kivuko hicho.

https://p.dw.com/p/1GuSN
Kenia Mombasa Fähre
Feri iliowabeba maelfu ya watu Mjini MombasaPicha: DW/E. Ponda

Hali hii imekwamisha kabisa usafiri kati ya kisiwa cha mji wa bandari wa Mombasa na maeneo ya Kusini mwa Kenya hadi nchi jirani ya Tanzania.

Watu kadhaa walijeruhiwa wakati walipojaribu kusongamana ndani ya feri moja iliyotolewa na halmashauri ya huduma za feri ili kujaribu kupunguza msongamano wa watu waliotaka kuvuka kuelekea makazini mwao asubuhi na mapema.Hata hivyo idara ya usalama mjini Mombasa haikutoa idadi kamili ya majeruhi.

“Watu walikanyagana sana, na sielewi serikali yetu inafikiria nini kuhusu maisha ya wakaazi wa mtaa wa Likoni. Maisha yao yamo hatarini kila kukicha kwa sababu ya feri hizi kukwama mara kwa mara” alisema Juma Kinyongo makaazi wa kitongoji cha Likoni.

Watumiaji wa huduma za feri hizo wanaotembea kwa miguu hawalazimiki kulipa ada yoyote, ingawa wafanyi biashara wanaosafirisha bidhaa kwa kutumia mikokoteni,hugharamika ada ya shilingi 60 hadi 100 kuvukisha bidhaa hizo, na tatizo hili hapana shaka lilikuwa ni pigo kubwa.

Kenia Mombasa Fähre
Watu katika kivuko cha feri cha likoni mjini MombasaPicha: DW/E. Ponda

“Hili sanduku moja ya nyanya nalipishwa shilingi 100 na nikivuka upande wa pili lazime nigharamike kiasi cha shilingi 60 kubeba mzigo hadi kwenye duka langu sasa bidhaa hizi zitaharibika kwa sababu hakuna usafiri, hii ni hasara kubwa” anasema mfanyi biashara Bakari Mavuno.

Mililolongo mirefu ya magari inayofikia kilomita moja kila upande wa kivuko hicho ilishuhudiwa na kukwamisha kabisa shughuli za kibiashara hasa malori yanayosafirisha mizigo kuelekea nchini Tanzania.

Wengi waathirika kufuatia feri ya kivuko cha Likoni kukwama

Idadi kubwa ya watalii waliokuwa wakienekea katika hoteli nyingi za kitalii zilizoko kusini mwa jji wa Mombasa pia walikwama huku wale waliokuwa wakielekea kuabiri ndege katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi wakilazimika kufutilia mbali safari zao.

Huduma za feri hizi ni muhimu kwa maisha ya wakaazi wengi, ukitaka kusafiri kwenda Tanzania lazima utumie kivuko hiki, Sasa angalia tatizo lililopo sasa, limekwamisha shughuli zote, nani wa kulaumiwa, bila shaka ni serikali”.. Anasema Saada mfanya biashara mmoja kutoka nchi jirani ya Tanzania.

Kivuko hiki cha Likoni ni muhimu kwa shughuli za kitalii kwani na mara nyingi tatizo hili linalopotokea huathiri pakubwa sekta ya utalii katika pwani ya Kenya.

Kenia Mombasa Fähre
Umati mkubwa wa watu uliokwama baada ya feri kuharibika mjini MombasaPicha: DW/E. Ponda

Maafisa polisi waliopelekwa kulinda usalama katika eneo hilo walikuwa na kazi ngumu ya kuongoza magari na msongamano ya watu hii si mara ya kwanza tatizo hili kutokea na watumiaji wa kivuko hiki wanalalamika kuwa wiki haiwezi kwisha bila ya visa vya kukwama kwa feri kati kati ya bahari au kuharibika kwa feri hizo kuripotiwa. Wanaulaumu usimamizi mzima wa halmashauri hiyo kwa kuzembea kazini.

Hata hivyo halmashauri hiyo inasema kuwa feri tatu zilipata matatizo usiku wa kuamukia leo Jumatatu, na kukwamisha kabisa huduma hizo.

“Juhudi zote zinafanya kuhakikisha kuwa huduma hizo zinarejesha haraka iwezekanavyo” anasema mkurugenzi wa halmashauri ya huduma za feri Hassan Musa

Kivuko hiki cha Likoni ninauwezo wa kuwahudumia zaidi ya abiria elfu 300 na magari 600 kwa siku. Serikali ya Kenya imetangaza mipango ya kujenga barabara nje ya kivuko hicho kuunganisha moja kwa moja na pwani ya kusini, ingawa mradi huu haujang'oa nanga.

Mwandishi: Eric Ponda

Mhariri: Daniel Gakuba