1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hu Jintao Urusi

26 Machi 2007

Rais Hu jintao wa China yuko nchini Urussi kwa ziara ya siku tatu. Rais Hu atakuwa na mkutano muhimu na rais wa Urusi Vladmir Putin katika suala la nishati.

https://p.dw.com/p/CHHV
Rais Jintao wa China
Rais Jintao wa ChinaPicha: AP

Katika kipindi hicho cha siku tatu cha ziara ya rais wa China,maafisa kutoka pande zote mbili Urussi na China wanatarajiwa kufunga mikataba ya kibishara yenye thamani ya dolla bilioni 4 pamoja na kuzungumzia mpango wa kinuklia wa Iran na Korea kaskazini.

Lakini wadadisi wa mambo wanasema cha muhimu kabisa kwenye ziara hiyo kwa upande wa China ni suala la nishati ambapo nchi hiyo inatafuta kupata hakikisho la kupata ongezeko la mafuta na gesi kutoka Urussi ambayo ni mzalishaji mkubwa wa nishati duniani.

Itakumbukwa ya kwamba mwezi uliopita rais Hu alifanya ziara ya siku 12 katika mataifa manane ya Afrika.Ziara hiyo ililenga hasa kuimarisha uwekezaji wa China kwenye mali asili ya bara hilo pamoja na kujipatia mafuta katika nchi yenye mgogoro ya Sudan.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Urussi ni kwamba makubaliano muhimu kabisa yatakayofikiwa wakati wa ziara hii ya bwana hu nchini humo ni juu ya mkataba kati ya urussi na makampuni ya reli ya China ambayo yataongeza kiwango cha usafirishaji wa mafuta ghafi hadi China.

Katika mwaka wa 2006 Urussi ilisafirisha tani milioni 15 za mafuta ghafi nchini China ambapo tani milioni 11 miongoni mwazo zilisafirishwa kwa njia ya reli.

Aidha mipango ya kuimarisha usafirishaji kwa njia ya meli imezusha wasiwasi kwamba usafirishaji katika mataifa ya magharibi huenda ukaathirika.

Ziara ya bwana Hu jintao pia inatarajiwa kugusia juu ya wasiwasi wa China kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Seberia hadi chanzo cha mafuta cha Daqing huko China.

Hapo kesho jumanne Marais Hu na Putin watazindua maonyesho makubwa ya vitu kutoka China ndani ya Kremlin.

Rais hu baadae atasafiri katika mkoa wa Tatarstan ambako kunakaliwa na idadi kubwa ya waislamu katikati ya Urussi na ambako kuna maeneo mengi ya mafuta jambo ambalo linawavutia wawekezaji wengi wa kigeni.

Marais Hu Jintao na Putin wanatarajiwa kuzungumza pia juu ya ushirikiano wao wa kidiplomasia ambao umeonekana kufanana katika kuyatatua masuala ya migogoro ya Nuklia ya Korea kaskazini na Iran.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema huenda viongozi hao wakashauriana juu ya msimamo wa kuchukua endapo maji yatazidi unga kwenye mgogoro wa Iran.