1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hosni Mubarak ahukumiwa kifungo cha maisha jela

Mohamed Dahman2 Juni 2012

Mahakama nchini Misri imemhukumu Rais wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak kifungo cha maisha gerezani baada ya kumkuta na hatia ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji wakati wa vuguvugu la kuupinga utawala wake.

https://p.dw.com/p/156yU
In this video image taken from Egyptian State Television, 84-year-old former Egyptian president Hosni Mubarak is seen in the defendant's cage as a judge reads the verdict in on charges of complicity in the killing of protesters during last year's uprising that forced him from power, in Cairo, Egypt, Saturday, June 2, 2012. Egypt's ex-President Hosni Mubarak has been sentenced to life in prison after a court convicted him on charges of complicity in the killing of protesters during last year's uprising that forced him from power. (Foto:Egyptian State TV/AP/dapd) EGYPT OUT
Urteilsverkündung Hosni Mubarak ÄgyptenPicha: dapd

Wakili mwandamizi katika kundi la mawakili wanaomtetea Mubarak ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kiongozi huyo wa zamani ambaye amepelekwa gerezani mjini Cairo baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Habari zinasema kwamba baada ya helikopta iliokuwa imemchukuwa Mubarak kutua kwenye kitengo cha hospitali cha gereza la Tora mjini Cairo kiongozi huyo wa zamani wa Misri aligoma kuteremka kwenye helikopta hiyo.

Afisa mmoja wa usalama amekaririwa akisema kwamba '' Alikuwa akilia na aligoma kushuka kwenye helikopta. Maafisa wa usalama ilibidi watumie muda kumshawishi ashuke kwenye helikopta hiyo na kuingia gerezani."

Waziri wake wa Mambo ya Ndani naye ahukumiwa kifungo hicho hicho

Waziri wa mambo ya ndani wa utalawa wa Mubarak, Habib al- Adly pia amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa mauaji hayo ya waandamanaji. Makamanda sita wa zamani wa polisi wameachiwa huru.

Madai ya rushwa yaliokuwa yakiwakabili watoto wa kiume wa Mubarak, Alaa na Gamal yalifutwa kutokana na kumalizika kwa muda wa kipindi ambapo kwayo hatua ya kisheria ilistahiki kuchukukiwa na rais huyo wa zamani pia amefutiwa mojawapo ya madai ya kesi za rushwa.

Kulizuka vurugu nje ya mahakama mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo huku kukiwa na mayowe ya''Batili,Batili" na sauti nyengine zikitaka mahakama iadhibiwe. Mawakili wenye hasira waliliambia shirika la habari la AFP kwamba wana hofu Mubarak ataonekana hana hatia katika rufaa ya kupinga hukumu hiyo.

Raia mjini Cairo baada ya hukumu ya Rais Hosni Mubarak
Raia mjini Cairo baada ya hukumu ya Rais Hosni MubarakPicha: dapd

Yasser Bahr wakili mwamdamizi wa jopo la mawakili linalomtetea Mubarak amesema watakata rufaa kutokana na hukumu hiyo kuwa na kasoro nyingi za kisheria kutoka kila pembe.

Alipoulizwa iwapo kuna uwezekano wa Mubarak kushinda rufaa hiyo Bahr amesema watashinda kwa asilimia milioni moja.

Mubarak alievalia miwani ya jua alikuwa amefumbata mikono yake na hakuonyesha hisia zake wakati Jaji Mkuu Ahmed Refaat alipokuwa akisoma hukumu hiyo.

Watoto wake Alaa na Gamal wakionekana wachovu walikuwa karibu watokwe na machozi waliposikia hukumu hiyo.

"Ni kulipiza kisasi kwa Wamisri kuona Mubarak na waziri wake wa ulinzi wakihukumiwa kifungo cha maisha lakini hukumu hiyo imezusha masuala mengi kuliko majibu" anasema Hussein Bahgat mkurugenzi wa shirika linaloshughulikia Haki za Watu Binafsi nchini Misri ambaye alikuwa nje ya mahakama pamoja na familia za wahanga.

Bahgat amesema inaonekana mahakama imeshindwa kupata ushahidi kwamba mauaji hayo yalifanywa na polisi na kwamba mahakama hiyo imewaona Mubarak na Adly kuwa na hatia kwa kushindwa kuzuwiya mauaji hayo.

Bahgat ambaye ni mwanaharakati na mwanasheria anayeheshimika amesema ni jambo la uhakika kwa asilimia 100 kwamba kutakuwepo na rufaa ambayo mahakama itaamuru kusikilizwa upya kwa kesi hiyo.

Wakati wa kutowa hukumu hiyo Jaji Refaat alitowa taswira ya mbaya ya maisha chini ya utawala wa Mubarak akielezea shida zilizowasumbuwa wananchi wakati wa utawala wake wa miongo mitatu.Alielezea juu ya baadhi ya watu waliokuwa wakishinda njaa na hali ilivyo kwenye vitongoji duni.

Refaat amesema waandamanaji walioshiriki katika vuguvugu la uasi katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo maandamano yao yalikuwa ya amani na walikuwa tu wakidai haki, uhuru na demokrasia. Kulizuka mapambano nje ya mahakama hiyo baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo ambapo polisi ililazimika kutumia maguruneti ya mshtuko kuudhibiti umma.Maelfu ya wananchi wa Misri wamiminika mitaani kutaka Mubarak anyongwe.

Mubarak mwenye umri wa miaka 84 dikteta pekee alieangushwa katika Vuguvugu la Majira ya Machipuko ya Nchi za Kiarabu kushtakiwa mwenyewe akiwa yupo mahakamani,Adly na watu wengine sita walikuwa wanakabiliwa na mashtaka kuhusiana na kuamuru mauaji ya watu wanaokadiriwa kufikia 850.

Kiongozi huyo wa zamani wa Misri na watoto wake Alaa na Gamal na mshirika wao wa biashara Hussein Salem aliekimbilia Uhispania pia walikuwa wakishtakiwa kwa madai ya kupokea hongo.

Mubarak alikuwa akituhumiwa kwa kuiuzia Israel gesi ya asili kwa bei ya chini kuliko ile ilioko kwenye masoko.

Hali ya usalama Misri

Polisi 5,000 na wanajeshi 2,000 wamemwagwa kuweka usalama katika mahakama na Chuo cha Polisi kilioko katika viunga vya Cairo ambapo kwayo Mubarak alichukuliwa kwa helikopta akitokea hospitali ya kijeshi.

Misri imekuwa ikitawaliwa na utawala wa kijeshi tokea Mubarak alazimishwe kujiuzulu hapo tarehe 11 mwezi wa Februari mwaka jana kufuatia siku 18 za maandamano ya taifa zima kupinga utawala wake.

Askari wakiwa katika Doria mjini Cairo
Askari wakiwa katika Doria mjini CairoPicha: dapd

Hukumu hiyo inakuja wiki mbili tu kabla ya kufanyika kwa marudiio ya uchaguzi wa rais ambao utampambanisha waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Mubarak, Ahmed Shafiq na mgombea wa chama cha Udugu wa Kiislam Mohammed Mursi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Stumai George