1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande na Obama kuliangamiza kundi la Dola la Kiislamu

Admin.WagnerD25 Novemba 2015

Ufaransa na Marekani zimeahidi kuimarisha mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, IS, zikiihimiza Urusi kujiunga na juhudi za kimataifa kuutanzua mgogoro wa Syria.

https://p.dw.com/p/1HCBX
USA, Francois Hollande und Barack Obama
Picha: Reuters/C. Barria

Rais Obama ameahidi kuiunga mkono kikamilifu Ufaransa katika vita dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, huku shinikizo likizidi kutoka kwa Ufaransa kushirikiana na Urusui nchini Syria. Haya yamejitokeza baada ya rais wa Ufaransa Francois Hollande kukutana na rais wa Marekani Barack Obama katika ikulu ya mjini Washington hapo jana. (24.11.2015)

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Obama amesema kundi hilo la kigaidi na itikadi zake za mauaji ni kitisho kikubwa na haliwezi kuvumiliwa. Obama ametoa wito kundi hilo liangamizwe kabisa kupitia ushirikiano.

"Tunapoendelea kuwa waangalifu, hatuwezi na katu hatutokubali kuwa waoga. Hatutakubali hofu itugawe kwa kuwa hivyo ndivyo magaidi wanavyoshinda. Tutashinda, na makundi kama ISIL yatashindwa. Tukisimama pamoja na washira wetu kama Ufaransa tutaendelea kuonyesha uongozi bora kabisa wa Marekani."

Rais Obama aidha amesema Marekani imekuwa ikitoa taarifa za kijasusi kuisaidia Ufaransa kuratibu mashambulizi yake nchini Syria na itaongeza ushirikiano huo.

Marekani na Ufaransa kuunda mkakati wa pamoja

Kwa upande wake rais Hollande amesema mzozo wa Syria unaliathiri moja kwa moja bara la Ulaya, kutokana na kitisho cha ugaidi na wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbia mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na vikosi vya serikali na ukatili wa kundi la Dola la Kiislamu, Daesh. Hata hivyo amefutilia mbali uwezekano wa kutuma wanajeshi wa ardhini nchini Syria, lakini akasema Ufaransa inawaunga mkono wapiganaji katika miji ya Ramadi na Mosul nchini Iraq.

"Leo tulitaka kubadilishana mawazo kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi kila mahala na wakati wote. Tulitaka pia kuumbia ulimwengu hatutawaruhusu wanaotaka kuharibu tulichokijenga, kizazi baada ya kizazi. Hawatoweza kuuharibu ulimwengu."

Frankreich Luftwaffe Kampfjets
Ufaransa inaimarisha mashambulizi dhidi ya Dola la KiislamuPicha: picture alliance/dpa/Ecpad Handout

Ziara ya Hollande mjini Washington ni sehemu ya mchakato wa kidiplomasia kuishawishi Marekani na mataifa mengine kuimarisha juhudi kulichakaza kabisa kundi la Dola la Kiislamu lililodai kuhusika na mashambulizi ya Novemba 13 mjini Paris ambapo watu 130 waliuliwa.

Hollande alisema baada ya mkutano wake na Obama kwamba Ufaransa na Marekani zimekubaliana kuanzisha mkakati wa pamoja, zikiwemo juhudi mpya za kuilenga mitandao ya fedha ya wanamgambo wa kundi hilo, kuyakomboa maeneo wanayoyadhibiti, kuimarisha mapambano nchini Syria na Iraq na kuongeza kubadilishana taarifa za kijasusi.

Kiongozi huyo wa Ufaransa atakutana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Paris leo na anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow hapo kesho, kabla kufanya mazungumzo na rais wa China Xi Jinping mjini Paris Jumapili ijayo.

Mwandishi:Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman