1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Hofu yatanda Kenya baada ya mashambulizi ya bomu kwenye disko

Raia nchini Kenya wameingiwa na hofu na polisi imewataka kuchukua hatua za tahadhari zaidi kufuatia mripuko uliotokea usiku wa kuamkia leo (24.10.2011) katika klabu moja ya usiku jijini Nairobi.

Jeshi la Kenya likielekea Somalia.

Jeshi la Kenya likielekea Somalia.

Watu wapatao 13 walijeruhiwa kwenye mripuko huo uliotokea mwendo wa saa 7.30 katika Baa ya Mwaura's Pub iliyoko barabara ya Mfangano mjini Nairobi. Duru za Hospitali Kuu ya Kenyatta zimedokeza kwamba kufikia sasa majeruhi wawili bado wako hospitali wakiendelea na matibabu ilihali 11 wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Hata hivyo, serikali imesema bado kwamba haijabainika iwapo watu waliotekeleza mashambulizi hayo wana uhusiano na kundi la Al-Shabaab.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Chuo cha Mafunzo ya Maafisa wa Upepelezi wa Jinai mjini Nairobi, Kamishna wa Polisi, Mathew Iteere, amefutilia mbali hofu kwamba shambulizi hilo lilitekelezwa na wanamgambo wa kundi la Al-Shabbab kutoka Somalia.

Helikopta ya jeshi la Kenya ikiruka mpakani mwa nchi hiyo na Somalia.

Helikopta ya jeshi la Kenya ikiruka mpakani mwa nchi hiyo na Somalia.

“Hakuna aliyedai kuhusika na shambulizi hilo kwani mtu aliyeingia na guruneti hilo ndani ya baa hakuonekana na mtu yeyote. Hakuna mtu anayeweza kusema kwamba alimwona mtu huyo”. Amesema Iteere, ingawa amewatahadharisha wananchi kuwa macho zaidi.

Kufuatia shambulizi hilo, usalama umeimarishwa mjini Nairobi na miji mingine mikubwa kote nchini. Tahadhari zaidi imewekwa katika hoteli, mikahawa na sehemu za burudani ambako kuna mikusanyiko mikubwa ya watu.

Wananchi wana wasiwasi kufuatia tukio hilo huku wengine wakitoa mwito kwa serikali iimarishe usalama zaidi.

Wiki iliyopita, kundi la Al-Shabaab lilitishia kufanya mashambulizi ndani ya ardhi ya Kenya kufuatia hatua ya majeshi ya Kenya kuingia nchini Somalia kuwasaka wanamgambo hao walio na uhusiano na kundi la magaidi la Al-Qaeda,  hali ambayo ilizua wasi wasi mkubwa miongoni mwa Wakenya.

Viongozi wa nchi, akiwemo Rais Mwai Kibaki na waziri Mkuu Raila Odinga, wamewahi kuwasihi wananchi kuwa macho zaidi na "kuhakikisha kwamba tunawatambua watu walio na nia mbaya miongoni mwetu.”

Mashambulizi hayo yamefanyika huku, vikosi vya jeshi la Kenya vikiendelea kukabiliana na waasi wa kundi la Al-Shabaab nchini Somalia.

Hatua ya Jeshi la Kenya kuingia ndani ya Somalia kuwasaka waasi wa kundi la Al-Shabaab ilifuatia msururu wa utekaji nyara katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kwa raia wa kigeni huko Lamu na maafisa wa mashirika ya misaada katika kambi ya wakimbizi ya Daadab majuma mawili yaliyopita.

Ripoti: Alfred Kiti. Mhariri: Josephat Charo
 • Tarehe 24.10.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12y1f
 • Tarehe 24.10.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12y1f