1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hatima ya hifadhi ya Julian Assange leo

Ecuador itatoa uamuzi leo juu ya kumpa hifadhi ya kisiasa mwanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks Julian Assange uamuzi ambao unaweza kusababisha mvutano wa kibalozi baina ya nchi hiyo na Uingereza.

default

Assange / Ecuador

Assange, raia wa Australia alipata umaarufu duniani baada ya mtandao wake wa Wiki Leaks kuchapisha nyaraka za siri ambazo zinazidhalilisha serikali mbalimbali hasa Marekani mwaka 2010.

Julian Assange

Julian Assange

Lakini katika kisa hiki, Assange anatakiwa nchini Sweden kwa ajili ya kuhojiwa kutoka na shutuma za kufanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia. Anatafutwa na yuko kwenye ubalozi wa Ecuador mjini London alikokimbilia tangu mwezi Juni mwaka huu.

Ecuador hapo jana iliishambulia Uingereza na kitisho ilichokitoa cha kuuvamia ubalozi huo ili imkamate Assange. Nao mtandao wa WikiLeaks umesema kuwa kitendo hicho kitakuwa ni cha chuki na kilichopitiliza na kisichoendana na mazingira.

Hofu ya Assange kuhusu kupelekwa Sweden

Assange mwenye umri wa miaka 41 anahofia kuwa atahamishwa kutoka Sweden na kupelekwa Marekani ambako anaweza kushitakiwa kwa kitendo cha mtandao wake kuvujisha siri za taifa hilo kuhusu masuala ya kisiasa juu ya vita vya Iraq na Afghanistan.

Kuvujishwa huku kwa nyaraka lilikuwa ni tukio kubwa kuwahi kuikumba Marekani. Macho yote sasa yameelekezwa Uingereza kutokana na jitihada zake za kutaka kumtoa Asange kwenye ubalozi wa Ecuador. Kama itafanya hivyo basi mzozo wa kibalozi utatokea.

Ricardo Patino, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Equador Assange

Ricardo Patino, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Equador

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ecuador Ricardo Patino amesema kuwa haikubaliki kwa polisi wa Uingereza kuingia kwenye ubalozi wao, lakini akasema kuwa nchi yake imeshafanya uamuzi na kuhusu hifadhi ya Assange na taarifa itatolewa baadae leo.

Patino anasema kuwa nchi yake imepokea kitisho cha maandishi kutoka Uingereza kinachosema kuwa itavamiwa kama haitampeleka Assange mikononi mwa nchi hiyo. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake inapinga vikali kitisho hicho.

Mtaalamu wa masuala ya sheria kwa watu wanaotafuta hifadhi Julian Knowles ameliambia shirika la habari la BBC kuwa mtu mwenye makosa yasiyo ya kisiasa hafai kupewa hifadhi

Mtizamo wa sheria ya kimataifa ya hifadhi

"Tukumbuke kuwa Julian Assange anatuhumiwa Sweden kwa kukiuka haki za binaadamu. Kupinga asikamatwe si sahihi kwani hii si kesi ya kisiasa ni kesi ya uhalifu. Sheria za kimataifa za kupata hifadhi zinaeleza kuwa nchi inapaswa kujiepusha na hifadhi za wahalifu kwa sababu zozote zile kwa kuwa mtu yeyote anayetuhumiwa kwa makosa ya uhalifu hahesabiwi kama mkimbizi." alisema Knowles.

Ubalozi wa Ecuador jijini London

Ubalozi wa Ecuador jijini London

Assange alikimbilia kwenye ubalozi wa Ecuador Juni 19 mwaka huu kukwepa kukamatwa na kpelekwa Sweden mpango ambao anauona kuwa ni njia ya kuitaka kumpeleka Mrekani akashitakiwe.

Hata kama atapata hifadhi hiyo, haijajulikana kama ataruhusiwa kuondoka kwenye ubalozi huo kwani polisi wa Uingereza wameuzunguka wakimwinda kumtia nguvuni kwa kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa mwaka 2010.

Ecuador imesema kuwa inazichunguza tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia ili kuweza kuamua kuhusu ombi la Asange kupewa hifadhi nchini humo.

Mwandishi: Stumai George/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com