1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE:Serikali yakiri kubana matangazo ya vituo vya kigeni

1 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCNU

Serikali ya Zimbabwe inakiri kuwa mawakala wake wanabana matangazo ya mashirika ya habari ya kigeni yanayodhaniwa kuponda serikali ya Rais Mugabe.

Kulingana na naibu waziri wa Habari wa Zimbabwe Bright Matonga raia wa kigeni kamwe hawatoruhusiwa kupeperusha matangazo bila idhini yao.

Suala hilo limezuka baada ya mbunge wa upinzani Willias Madzimure kuuliza kinachosababisha kubanwa kwa matangazo ya Shirika la habari la marekani Voice of Amerika.

Kituo chengine cha binafsi cha SW Radio Afrika kilitoa malalamiko yake mwaka jana kuwa mawakala wa serikali wanabana matanagzo yake.Kituo hicho kilicho na makao yake mjini London kilicho na sifa ya kupinga utawala wa Rais Mugabe kiliendesha shughuli zake katika hoteli moja mjini Harare kabla kufungwa mwaka 2002.

Hakuna vituo vyovyote vya redio vinavyotangaza nchini Zimbabwe japo sheria za utangazaji zilibadilishwa miaka 6 iliyopita.Sheria hizo mpya zilinuia kuruhusu vituo binafsi kutangaza na kushindana na redio ya serikali inayosikika kote nchini.

Serikali aidha inapendekeza sheria mpya itakayowezesha mawakala wa serikali kuunda kituo maalum cha kusikiliza mawasiliano ya simu vilevile kutazama barua pepe na fax zinazotumwa nchini humo.