1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE:Operesheni Dzikiza kuendelea kwa majuma matatu

18 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBhf

Serikali ya Zimbabwe inaongeza kasi hatua ya kuwaadhibu wafanyibiashara wote wanaokiuka agizo la kupunguza bei za bidhaa na huduma kwa nusu.Kwa mujibu wa waziri wa habari na utangazaji serikali ya Rais Robert Mugabe iliamua kuongeza muda wa kutekelezwa operesheni hiyo kwa jina Dzikiza kwani imeonyesha kuwa bei znarudi chini.

Wafanyibiashara na wazalishaji walilazimika kuongeza bei za bidhaa mara kadhaa kwa siku ili kupambana na mfumko wa bei za bidhaa unaoaminika kupita asilimia alfu 5.Hatua hiyo ilipelekea serikali kutoa agizo la kupunguza bei kwa nusu mwezi uliopita.

Yapata wafanyibiashara 3000 wamekamatwa na kuzuiliwa kwa kukiuka agizo hilo wengi wao wakitozwa faini.Kwa upande wao wafanyibiashara wanasisitiza kuwa bei zilizowekwa na serikali haziwezi kufidia gharama za uzalishaji jambo linalosababisha biashara ya magendo kushamiri.

Wakati huohuo Marekani inatangaza kupeleka tani alfu 47 za msaada wa chakula nchini Zimbabwe ili kukabiliana na uhaba wa bidhaa za matumizi.

Rais Mugabe aliyerudi madarakani tena mwaka 2002 anashikilia kuwa hataki mataifa ya magharibi kuingilia masuala ya nchi yake.Kiongozi huyo amepigwa marufuku kuingia Marekani na Umoja wa Ulaya.