1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas, Israel wasitisha mapigano Gaza

Bruce Amani
21 Julai 2018

Kundi la Hamas limetangaza kusitisha mapigano na Israel katika Ukanda wa Gaza, baada ya siku ya machafuko ambayo yalisababisha vifo vya mwanajeshi mmoja wa Israel na Wapalestina wanne

https://p.dw.com/p/31qoD
Palästina Aufräumen nach israelischem Luftangriff in Gaza
Picha: Reuters/S. Salem

Msemaji wa Hamas Fawzi Barhoum amesema kwenye Twitter kuwa makubaliano na Israel yamefikiwa kwa msaada wa Misri na Umoja wa Mataifa

Msemaji wa jeshi la Israel amesema hangeweza kuyajadili masuala ya kisiasa, lakini akasema Israel kwa sasa haifanya mashambulizi yoyote Gaza.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Jonathan Conriczs amesema jeshi la nchi hiyo tangu Ijumaa liliyashambulia maeneo 60, yakiwemo makao makuu matatu ya wapiganaji wa Hamas.

Jeshi la Israel lilisema mapema kuwa mashambulizi yake ya angani yalikuwa ya kujibu shambulizi la ufyatuaji risasi dhidi ya wanajeshi wake waliotumwa kusini mwa mpaka wa Gaza, ambako waandamanaji wa Kipalestina walikusanyika kwenye uzio.

Palästina Israel fliegt nach Schüssen auf Soldaten massive Luftangriffe in Gaza
Machafuko ya Gaza yameongezeka Picha: picture-alliance/AA/A. Amra

Wapalestina wanne waliuawa na wanajeshi wa Israel kufuatia makabiliano yaliyozuka, imesema Wizara ya Afya ya Gaza. Kwa mujibu wa Hamas, ambayo inadhibiti Ukanda wa Gaza, watatu kati ya waliouawa walikuwa wanachama wa Hamas.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov, ambaye hivi karibuni alishirikiana na Misri kupunguza mvutano katika kanda hiyo, aliziomba pande zinazohusika kujizuia na kuwa watulivu. Hapo jana Ijumaa, kulikuwa na maandamano mapya kwenye mpaka wa Gaza, huku Wapalestina wakichoma moto matairi, wakijaribu kuharibu uzio wa mpaka na Israel.

Wizara ya Afya ya Gaza inasema maandamano hayo yamesababisha vifo vya Wapalestina 146 na maelfu kujeruhiwa na wanajeshi wa Israel tangu mwishoni mwa mwezi Machi.

Wapalestina wanadai kumalizika kwa mzingiro wa Gaza ambao uliwekwa Zaidi ya miaka kumi iliyowekwa miaka kumi iliyopita, pamoja na haki ya kurejea kwenye eneo hilo ambalo walitimuliwa wakati Israel ilipoanzishwa mwaka wa 1948

Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa Misri ilituma onyo la mwisho kwa Hamas kutoka kwa Israel, likisema kuwa kama mashambulizi hayatasimama ifikapo wikiendi hii, itafanya mashambulizi mapya ya kijeshi katika ukanda wa pwani.

Hamas na Israel walipigana vita vilivyodumu siku 50 katika mwaka wa 2014. Kwa jumla, Wapalestina 2,250 waliuawa au wakafariki baadaye kutokana na majeraha wakati Waisrael 74 waliuawa katika mgogoro huo.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: John Juma