1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali iko vipi Kisumu kabla ya uchaguzi?

John Marwa7 Agosti 2017

Karibu kila gumzo mjini Kisumu linahusu uchaguzi pekee. Wananchi wamehakikishiwa usalama wakati wa upigaji kura na wameshauriwa kutotaharuki kufuatia mifuko 100 ya kuwatia wafu iliyopewa polisi.

https://p.dw.com/p/2hpuf
Kenia Wahlen
Picha: Reuters/M. Eshiwani

Huko magharibi mwa Kenya, utata umezuka mjini Kisumu baada ya baadhi ya wapiga kura kutopata ithibati ya kushiriki katika zoezi hili kupitia huduma ya ujumbe mfupi wa simu hadi sasa, ikiwa ni masaa machache kabla ya kura.

Hata hivyo Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi nchini Kenya imejiondelea lawama na kusema pia kuwa ithibati kupitia njia hiyo si thabiti, huku ikisema maandalizi yote ya uchaguzi yamekamilika kulingana na tume ya uchaguzi, na vyombo vingine vya dola.

Karibu kila gumzo mjini Kisumu linahusu uchaguzi pekee. Eneo hili likiwa ngome kuu ya upinzani nchini, wote hapa tuliowahoji wameelezea matumaini yao kuwa Kiongozi wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Amolo Odinga, almaarufu Baba atashinda.

Mfuasi wa Raila Odinga akibeba noti bandia yenye picha ya Raila Odinga
Mfuasi wa Raila Odinga akibeba noti bandia yenye picha ya Raila OdingaPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi mkuu wa uchaguzi katika Kaunti ya Kisumu, John Cox Lorionokou, maandalizi yote yameishakamilika.

Hata hivyo baadhi ya wapiga kura wamelalamika kuhusu kutothibitishiwa kupitia huduma ya ujumbe mfupi wa simu kuwa wataruhusiwa kupiga kura.

Msimamizi wa uchaguzi John Cox hata hivyo ameiondolea lawama tume na kushauri hawa wote kufika katika vituo vya kura ambapo itachunguzwa katika sajili zote za wapiga kura.

Pamoja na tume hii ya uchaguzi, vyombo vingine vya dola kama vile polisi na utawala vimesema kuwa viko tayari na kuhakikishia umma usalama wao wakati wa zoezi la uchaguzi.

Kamishna wa eneo la Nyanza, Wilson Njega, kadhalika ameiomba umma kutotaharuki baada ya mifuko 100 ya kuwatia wafu kutolewa kwa polisi na shirika moja lisilo ya kiserikali.

Wapiga kura wote wanahimizwa kupiga kura na vilabu vingi vya pombe pamoja na maduka madogo madogo ya pombe yamelazimishwa na umma kusimamisha uuzaji wa pombe kuanzia leo hadi mwisho wa zoezi hili kesho jioni ili watu wasilewe na kupitwa na kura.

Mwandishi: John Marwa/DW Kisumu

Mhariri: Mohammed Khelef