″Hakuna mtu yeyote anayetaka vita vya baridi vianzishwe upya″ | Magazetini | DW | 18.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Hakuna mtu yeyote anayetaka vita vya baridi vianzishwe upya"

Suala kuu kwenye kurasa za uchambuzi za magazeti ya Ujerumani hii leo ni mzozo wa kidiplomasia kati ya Uingereza na Urusi ambao chanzo chake ni kifo cha kachero wa zamani wa Urusi Alexander Litvinenko.

Uingereza imewafukuza nchini wanadiplomasia wanne wa Urusi ambao kwa mujibu wa serikali ni wafanyakazi wa idara za ujasusi za Urusi. Hii imetokea baada ya Urusi kukataa kumrejesha mshukiwa mkuu Andrei Lugovoi katika mauaji ya Litvinenko. Kwanza juu ya mvutano huu ni gazeti la “General-Anzeiger” la hapa mjini Bonn :

“Uingereza kusisitiza mshukiwa Lugovoi arejeshwe huko ni sawa. Kama serikali ya Uingereza inachukua msimamo mkali katika kisa hicho ni kwa sababu inaona kuwa nchi za Magharibi zinapaswa kupinga namna Vladimir Putin anavyotawala kwa mkono wa chuma. Kitu kinachostusha lakini ni kwamba Uingereza haiufikirii msimamo wa Urusi. Na juu ya hayo: Je, Uingereza ina mpango wowote vipi kuendelea katika suala hilo? Pamoja na kutaka serikali ya Urusi ijibu hatua ya Uingereza, hakuna mtu yeyote anayetaka vita vya baridi vianzishwe upya.”

Ni gazeti la “General-Anzeiger”. Kwa maoni ya mhariri wa “Allgemeine Zeitung” la mjini Mainz, hatua ya kuwafukuza wanadiplomasia wa Urusi kutoka Uingereza ni hatua iliyotarajiwa kutokea. Ameandika:

“Waziri mkuu mpya Gordon Brown anaweka ishara akiwaambia Warusi: Sisi tunajua mnafanya nini na hatukubali hata kidogo. Uamuzi wa Bw. Brown lakini si tu onyo kwa serikali ya Urusi, bali pia ni njia ya kuwaonyesha raia wa Uingereza kwamba waziri mkuu huyu ni wa aina gani. Bila shaka watampigia makofi, kwani kinyume cha raia wengine wa bara la Ulaya, Waingereza hawaiamini serikali ya Urusi.”

Na moja kwa moja tunaendelea na gazeti la “Stadt-Anzeiger” la kutoka Cologne. Limeandika:

“Kisa cha Litvinenko kimeanzisha mzozo ambao lazima ungetokea, yaani ule kati ya Urusi yenye serikali fidhuli na Ulaya ambayo inawakilishwa na Uingereza. Kuwafukuza wanadiplomasia hao wanne wa Urusi ni hatua ya kutoa ishara tu, kwani haiwezekani kuweka vikwazo vya kiuchumi kutokana na uhusiano wa kiuchumi wa karibu kati ya Mosko na London. Hata hivyo lakini, kutumia ishara pia ni kutuma ujumbe ulio wazi, yaani kwamba Urusi ikiwa na serikali kama hii ya leo haitapewa nafasi na Umoja wa Ulaya.”

Na hatimaye juu ya suala hili, gazeti la “Neues Deutschland” linataja wasiwasi wake juu ya hatua iliyoichukua Uingereza. Tunasoma:

“Namna Alexander Litvinenko alivyokufa ni vibaya sana. Bila ya kujali maoni tofauti juu ya afisa huyo wa ujasusi, kulifumbua fumbo juu ya mauaji haya ni lengo nzuri. Lakini kuwafukuza wanadiplomasia wa Urusi kutoka London hakutasaidia hata kidogo kwa sababu katiba ya Urusi, sawa na sheria katika nchi nyingi zaidi – hairuhusu mwananchi wake apelekwe nje akiwa ni mshukiwa.”

 • Tarehe 18.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHSO
 • Tarehe 18.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHSO