1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guinea ya Ikweta na Libya kufungua dimba kombe la Afrika

Sekione Kitojo21 Januari 2012

Kombe la mataifa ya Afrika linaanza rasmi leo Jumamosi baada ya matayarisho kwa ajili ya michuano hiyo yaliyofanywa na mataifa mawili wenyeji wa mashindano hayo Guinea ya Ikweta na Gabon

https://p.dw.com/p/13niH
Logo 2012 Africa Cup of Nations, Quelle: CAF ***Das Logo darf nur in Zusammenhang mit einer Berichterstattung über die Institution verwendet werden ***
Nembo ya kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2012Picha: CAF

Tamasha  kama  hili  kubwa  la  michezo  linalofanyika  kila  baada ya  miaka  miwili  haliwezi  kukamilika , hata  hivyo , bila  kuwa  na aina  yake  ya  utata, na  tamasha  la mwaka  huu  halina  tofauti.

Mara  hii  wakati  wa  kuelekea   kuanza  kwa  tamasha  hilo  mjini Bata  ambako  Guinea  ya  Ikweta  inakumbana  na  Libya   katika mchezo  wa  ufunguzi  kumekuwa  na   malalamiko  kutoka  Burkina Faso   na  Zambia  kuhusiana  na  malazi  huku  timu  zote zililazimika  kubadilisha  hoteli  walizopangiwa.

Tulipowasili  hapa , walituweka  katika  mgahawa . Ilikuwa  hata haina  hadhi  ya  hoteli. Hakuna  chumba  cha  video, hakua  chumba cha  mikutano. Kila  mara  inabidi  kufanya  ujanja  tu. Hivi  ndivyo kombe  la  Afrika  linavyokuwa, amelalamika  kocha  wa  Burkina Faso  Paulo Duarte.

Nadhani  watu  wanapaswa  kuwa  na  heshima  na  timu  ya  taifa ya  Zambia. Sio  mara  yetu  ya  kwanza  kufikia  katika  fainali  hizi, ameongeza  kocha  wa  Zambia  Herve Renard

Watayarishaji  wa  mashindano  hayo   ya  CAF  wamejibu  kwa kusema  kuwa   hoteli  ambazo  timu  zimepangiwa  zimechaguliwa kutokana  na  kura, ili  kuepuka  kutowatendea  haki  timu  yoyote.

Kama chakula  maalum  kilichoandaliwa  bila  ya  kuwa   na  mgeni maalum  tamasha  hili   la  soka  linafanyika  bila  ya  kuwapo mabingwa  mara  tatu  wa  fainali  tatu  zilizopita  Misri.

Mbali  na  Misri  vigogo  wengine  katika  soka  la  Afrika , Cameroon , Nigeria, Algeria  na  Afrika  kusini  pia  wameshindwa  kufuzu kuingia  katika  fainali  za  mwaka  huu.

Katika  timu  hizi  nne  vigogo  vya  soka , Ghana  ambayo  imefikia robo  fainali  ya  kombe  la  dunia   na  Cote D'Ivoire  ya  Didier Drogba  ni  timu  zinazoonekana  kuwa  na  uwezo  wa  kutoroka  na kombe  hilo, ambalo  limewapiga  chenga  kwa  muda  mrefu.

Didier Drogba of Ivory Coast in action during the Africa Cup of Nations match between Ivory Coast and Ghana in Cabinda, Angola, 15 January 2010. EPA/- EDITORIAL USE ONLY +++(c) dpa - Bildfunk+++
Nyota wa Cote D'Ivoire Didier DrogbaPicha: picture-alliance/dpa

Orodha  ya  timu  zilizoingia  fainali  ya  mwaka  huu  katika  kombe la  Afrika  inamaajabu  yake,  mojawapo  ni  Libya  ambayo imefanikiwa   kufuzu  kuingia  katika  fainali  hizi  mbali  ya  matatizo ya  kisiasa  na  vita  nchini  mwake , hali  iliyosababisa  kuondolewa madarakani  kwa  kiongozi  wa  muda  mrefu  wa  nchi  hiyo Mouammar  Gaddafi  na  hatimaye  kuuwawa.

Heko  pia  ziwaendee  Niger  na  Botswana , timu  hizi  mbili  ambazo zinaonekana  kuwa  ni  wanagenzi  pamoja  na  Guinea  ya  Ikweta ambayo  imeingia  katika  kinyang'anyiro  hicho  kutokana  na  kuwa mwenyeji  mwenza  wa  mashindano  hayo  wamejiweka  katika meza  kuu  ya  soka  la  Afrika  kwa  sasa.

Hata  hivyo  vyota  wa  soka  wa  zamani  katika  bara  la  Afrika wameonya  zile  ztimu  ambazo  zinaonekana  kuwa  na  uwezo  wa kulinyakua  kombe  hilo  kuwa  makini  na  timu  zinazoonekana  kuwa dhaifu  kama  Botswana  na  Niger  wakati  muda  unakaribia   wa kuanza  kwa  mashindano  hayo. Abedi  Pele, Ayew  wa  Ghana , Rogobert  Song  wa  Cameroon  na   Mustapha  Hadji  wa  Morocco wamekubali  kuwa  maelezo  kuwa  Cote D'Ivoire na  Ghana  zitafikia fainali  hapo  tarehe  12  February  ni  mapema  mno  na  kwamba kunaweza  kutokea  maajabu  kabla  ya  vumbi  kutua  katika  viwanja hivyo  nchini  Guinea  ya  Ikweta  na  Gabon.

Mwandishi : Sekione  Kitojo  / AFPE

Mhariri : Sudi  Menette