1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guardiola awekewa mbinyo

13 Septemba 2013

Wakurugenzi wa klabu ya Ujerumani Bayern Munich wamemwekea mbinyo kocha Pep Guardiola wakati mabingwa hao wakiingia katika kipindi cha wiki zenye kibarua kikubwa.

https://p.dw.com/p/19hHQ
Mkufunzi wa Bayern Pep Guardiola
Mkufunzi wa Bayern Pep GuardiolaPicha: picture-alliance/dpa

Bayern ni wa pili katika Bundesliga nyuma ya mahasimu Borussia Dortmund na wanaanza kutetea taji lao la Champions League dhidi ya CSKA Moscow Jumanne wiki ijayo. Kisha mchuano huo utafwatwa na mechi ya ugenini dhidi ya Schalke 04, mechi za nyumbani dhidi ya Hanover, tena katika kombe la Shirikisho, Wolfsburg katika ligi, na kisha Champions League ugenini nyumbani kwa Manchester Coty, kabla ya kupambana na Bayer Leverkusen katika Bundesliga. Mechi hizo zote katika kipindi cha wiki tatu.

Na licha ya ratiba hiyo ya kutia adabu, wasimamizi wa Bayern wanataraji kuwa timu yao itadhihirisha kuwa iko imara chini ya Guardiola jinsi tu ilivyokuwa chini ya mtangulizi wake Jupp Heynckes. Rais wa klabu Uli Hoeness anasema wanapaswa kuendelea na kasi ile ile jinsi walivyofanya msimu uliopita.

Naye Mwenyekiti Karl Heinz Rummenige pia anasema hawawezi kuwa na visingizio vyovyote..kwa sababu wako katika awamu ambayo hawawezi kamwe kukubali uzembe. Aliyasema haya akiangazia mchuano waliotoka sare ya goli moja kwa moja dhidi ya Freiburg katika mechi yao ya mwisho ya Bundesliga.

Guardiola tayari ameipa Bayern München kombe la UEFA Super Cup
Guardiola tayari ameipa Bayern München kombe la UEFA Super Cup, baada ya kuipiku ChelseaPicha: Alexander Hassenstein/Bongarts/Getty Images

Mkurugenzi wa Spoti Matthias Sammer pia hajawachwa nyuma, kwa sababu aliyataja matokeo hayo kuwa ya kukasirisha, baada ya Guardiola kukichagua kikosi hafifu. Bayern wana matatizo kadhaa ya majeraha, huku Mario Goetze, Thiago Alcantara, Javi Martinez na Jan Kirchoff wote wakiwa mkekani. Lakini wanataraji kuwa Bastia Schweinsteiger atarudi kikosini kupambana leo na Hanover.

Borussia Dortmund, timu pekee yenye rekodi ya asimilia 100 kufikia sasa msimu huu, inaialika Hamburg, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu majeruhi mpoland Jakub Blaszczykowski, aliyejeruhiwa wakati akitekeleza majukumu ya nchi.

Mshambuliaji Robert Lewandowski anatarajiwa kuwa shwari huku naye kiungo Marco Reus akirejea kikosini baada ya kukosa mechi ya Ujerumani ya kufuzu katika kombe la dunia dhidi ya Visiwa vya Faroe akiwa na maumivu ya tumbo.

Schalke 04 wanapasha misuli moto kwa mchuano wao wa Jumatano wiki ijayo wa Champions league dhidi ya wageni Steaua Bucharest, kwa kuangushana na Mainz na wanataraji kuwa mshambulizi wao Mholanzi Klaas-Jan Huntelaar atarejea hivi karibuni kutoka mkekani. Katika mechi nyingine za leo, Bayer Leverkusen v VfL Wolfsburg, Werder Bremen v Eintracht Frankfurt na Augsburg v Freiburg. Hapo kesho, Jumapili, Hoffenheim v Borussia Moenchengladbach, wakati nao Eintracht Braunschweig v Nuremberg

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman