1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gordon Brown kutohudhuria mkutano

Ramadhan Ali20 Septemba 2007

Gordon Brown atishia kutohudhuria mkutano wa kilele ujao baina ya Ulaya na Afrika ikiwa rais Mugabe wa Zimbabwe atahudhuria.

https://p.dw.com/p/CHjF
Waziri mkuu Gordon Brown
Waziri mkuu Gordon BrownPicha: AP

Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown ametishia kuususia mkutano ujao wa kilele kati ya Umoja wa ulaya na Afrika ikiwa rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atahudhuria.Brown ametoa pia mwito kwa viongozi wa ulimwengu kuongeza shinikizo kwa serikali ya Mugabe.

Katika makala kwenye toleo la leo la gazeti la INDEPENDENT la Uingereza, waziri mkuu Gordon Brown ,amemtuhumu rais Mugabe kuwatendea maovu wananchi wake binafsi na kuwatesa watu na kueneza vitisho nchini kwa wapinzani wake wa kisiasa.

Bw.Brown akaandika zaidi kwamba ikiwa rais Mugabe atahudhuria mkutano ujao wa kilele wa desemba 8-9 mjini Lisbon,basi Mugabe atauchafua mkutano huo,atageuza macho ya wajumbe kutoka mada hasa za kuzungumzwa na katika hali kama hiyo,kushiriki kwake Brown si jambo barabara-alisema.

Waziri mkuu wa Uingereza akautaka Umoja wa Ulaya kutekeleza marufuku yake ya vikwazo vya usafiri kwa Mugabe na akashauri tume ya haki za binadamu ya UM ipelekwe Zimbabwe.

Wakati lakini, waziri mkuu Brown anajaribu kuutenga utawala wa Zimbabwe na ulimwengu,wakati huo huo akitarajiwa kutangaza hii leo msaada zaidi wa kiuchumi kwa Zimbabwe.

Uingereza, ambayo ni mfadhili mkubwa wapili kwa Zimbabwe itaipa Zimbabwe dala milioni 16 zaidi za msaada kupitia Mpango wa Chakula Ulimwenguni –World food Programme.

Siasa kali za Mugabe zinalaumiwa kuwa chanzo cha msukosuko wa miaka 8 sasa wa kiuchumi humo nchini uliofuatana na ukosefu mkubwa wa kazi,ughali wa maisha ,ukosefu wa kazi wa hadi 80% na upungufu mkubwa wa chakula.

Rais Mugabe mara kwa mara akiilaumu kambi ya nchi za magharibikuwa shabaha yao hasa ni kuibadili serikali yake na kwamba inapanga njama na upinzani nchini kuifikia shabaha hiyo.Mugabe pia analaumu vikwazo vya kiuchumi vya nchi za magharibi vilivyowekewa wajumbe wa chama chake tawala kuwa sababu pia ya misukosuko ya Zimbabwe.

Rais Mugabe amepigwa marufuku ya usafiri katika nchi za Umoja wa ulaya ,lakini marufuku hayo yaweza ya kusitishwa kwa muda kumwezesha ahudhurie mkutano huo wa kwanza wa kilele tangu 2000 baina ya UU na UA hapo desemba mjini Lisbon,Ureno.

Waziri mkuu Brown wa uingereza amesema na ninamnukulu,

“Rais Mugabe ni kiongozi pekee wa Afrika kuwekewa kikwazo cha usafiri katika UU.Kuna sababu yake-nayo ni jinsi anavyowatendea wananchi wake.”

Gordon Brown aliandika katika makala yake hiyo kuwa ataunga mkono juhudi zinazofanywa na majirani wa Zimbabwe pamoja nao Afrika Kusini na Tanzania kuzungumzia kurejea demokrasi nchini Zimbabwe ,koloni la zamani la Uingereza.