1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gordon Brown Kujiuzulu Septemba

Kabogo Grace Patricia11 Mei 2010

Waziri huyo mkuu wa Uingereza atajiuzulu kama kiongozi wa chama chake cha Labour.

https://p.dw.com/p/NKqq
Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown amesema atajiuzulu kama kiongozi wa chama chake cha Labour mwezi Septemba mwaka huu wakati chama hicho kikitafuta uwezekano wa kuunda serikali ya muungano na chama cha Liberal Democrats.

Akitangaza uamuzi huo katika Ikulu ya 10 Downing Street, Bwana Brown alisema hakutaka kuwa katika njia ya kuunda serikali ya muungano kati ya Labour na Liberal Democrats. Ameongeza kusema kuwa amechukua uamuzi huo baada ya chama chake kufanya vibaya katika uchaguzi mkuu wiki iliyopita.

Matamshi hayo ya Bwana Brown yanaonekana kama hatua ya kuongoza njia ya kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya muungano kati ya chama cha Conservative na Liberal Democrats. Chama cha Conservative kilipata viti vingi katika uchaguzi huo, lakini viti hivyo havitoshi kukifanya chama hicho kuunda serikali peke yake.