1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Goodluck Jonathan aongoza uchaguzi Nigeria

Sekione Kitojo18 Aprili 2011

Rais Goodluck Jonathan anaonekana kuelekea kupata ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi mkuu wa rais nchini Nigeria, ambapo hakutakuwa na haja ya kuwa na duru ya pili ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/10vPC
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan akipiga kura katika uchaguzi wa rais katika mji wa Otuoke, Nigeria, Jumamosi April 16, 2011.Picha: AP

Nigeria  imeweza  kuendesha  kwa  mafanikio  zoezi  la  uchaguzi  wa rais  hapo Jumamosi  baada  ya  kufanikisha  uchaguzi  wa  bunge hapo  tarehe  9  mwezi  huu. Waangalizi  wa  uchaguzi  huo   pamoja na   wapiga  kura  wengi  wameonyesha  kuridhishwa   na  hali inayoendelea  ya  amani  na  utulivu  katika  zoezi  hili  la  uchaguzi na  jinsi  ulivyotayarishwa.

Rais  Goodluck  Jonathan  anaongoza  akiwa  hadi  sasa  amepata kiasi  cha  kura  milioni  22  zilizohesabiwa  kutoka  majimbo 35  kati ya  36  nchini  Nigeria.

Tume  huru  ya  uchaguzi  bado  inasubiri  matokeo  kutoka  katika jimbo  moja  pamoja  na  baadhi  ya  maeneo. Chama  cha  rais Jonathan  cha Peoples  Democratic Party, PDP,  kimepata   kura nyingi  katika  maeneo  ya  kusini  ambako  ndiko  anakotoka  pamoja na  kusini  magharibi , kusini  mashariki  na  kaskazini  kati.

Idadi  kubwa  ya  wapigakura  milioni  73.5  ambao  wamejiandikisha kupiga  kura   walijitokeza  siku  ya  Jumamosi  katika  uchaguzi  huo wa  rais.

Mpinzani  mkuu   wa  Jonathan, kiongozi  wa  zamani  wa  kijeshi Muhammadu  Buhari, amepata   hadi  sasa   kura  milioni  10.8 kutoka  katika  eneo  la  kaskazini  ambako   ni  ngome  yake. Mgombea  kijana  zaidi   kati  ya  wagombea  watatu  wa  kiti  cha urais, Nuhu  Ribadu   wa  chama  cha  Action Congress  of  Nigeria ACN, amepata  kura  milioni 2.2.

Nigeria Wahlen Muhammadu Buhari Oppositionsparteiführer ANPP
Muhammadu Buhari wa chama cha upinzani cha ANPP All Nigeria People's Party.Picha: AP

Buhari  ambaye  amegombea  kiti  hicho  kwa  tiketi  ya  chama  cha Congress  for  Change, amesema   kuwa   hatapinga  matokeo  ya uchaguzi  mahakamani, lakini  chama  chake  kinaweza  kufanya hivyo  iwapo  kitapenda.

Aligombea  akashindwa   katika  uchaguzi  wa  mwaka  2003  na 2007  dhidi  ya  chama  tawala  cha  Peoples Democratic, PDP.

Kushindwa  kwa  ushirika  baina  ya  chama  cha  CPC  na  Action Congress  of  Nigeria ACN  kumesababisha  Jonathan  kushinda katika  eneo  la  kusini  magharibi  ya  Nigeria, kufuatia  mashauriano ya  muda  mrefu   na  wadau  ili  wamuunge  mkono. Muungano  wa chama  cha  CPC  na  ANC  ulishindikana  kutokana  na   madai  ya masharti   ambayo  hayakuweza  kukubalika   kwa   pande zote . Ulinzi  uliongezwa katika  kituo  cha  kupokea  matokeo  mjini  Abuja , mji  mkuu  wa  nchi  hiyo,  ambapo  viongozi  wa  idara  mbali  mbali za   vyuo  vikuu  walitumika  kama  maafisa  wa  kutuma  taarifa za  matokeo  kutoka  katika  majimbo  36  na  miji  mikuu  ya majimbo,  ambapo  huo  ni  utaratibu  mpya  ambao  unatarajiwa kuleta  hali  ya  kuaminika  na  kuhakikisha  uwazi  wa  zoezi  la uchaguzi. Mkuu  wa ujumbe  wa   waangalizi  kutoka  umoja  wa Ulaya , Alojz Peterle  ameusifu  uchaguzi  huo  siku  ya  Jumamosi, na  siku  moja  baadaye  kundi  la  waangalizi   wa  ndani  wa  Nigeria pia  lilifanya  hivyo. Mradi  wa  hesabu  ya  haraka , 2011 Swift Count, ulituma   wawakilishi  karibu  1,500  katika  uchaguzi  wa majimbo. Wakili  Dafe Akpedeye  alitoa  matokeo  ya  kundi la  mradi huo  mjini  Abuja.


Mradi  wa   hesabu  ya  haraka   umeweza  kufanyakazi  katika nchi  nzima, na  kuwezesha   kuwapa  fursa  halisi  wananchi kuweza  kutimiza  haki  yao  ya  kushiriki  katika  zoezi hili. Hatua  za  uchaguzi   zilikwenda  vizuri  kama  ilivyokuwa  katika uchaguzi  wa  bunge wiki  moja  kabla.

Hata  hivyo  ghasia  za  hapa  na  pale  zimetokea  katika  sehemu  za  kaskazini  za Nigeria  usiku  wa  kuamkia  leo  wakati  rais  Goodluck  Jonathan akielekea  kupata  ushindi  katika  duru  ya  kwanza  ya  uchaguzi  wa rais, wameeleza  polisi  na  wakaazi  wa  eneo  hilo. Madai  ya  wizi wa  kura  yamesababisha   ghasia  mitaani  katika   baadhi  ya sehemu  za  majimbo  ya  Kaduna  na  Sokoto. Hapo  mapema majumba  yalichomwa  moto  katika  jimbo  la  Bauchi  na  Gombe.

Mwandishi : Thomas Mösch / ZR / Sekione  Kitojo

Mhariri : Mohammed  Abdul-Rahman