George W. Bush azindua kitabu chake. | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

George W. Bush azindua kitabu chake.

Bw Bush asema hajafikiria kuomba msamaha kutokana na maamuzi wakati wa utawala wake.

default

Tayari kuna nakala milioni 1.5 za kitabu hicho.

Kwa takriban miaka miwili baada ya kuondoka madarakani, rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush amekuwa kimya sana.

Hata hivyo kuzinduliwa kwa kitabu chake kiitwacho ‘Decision Points’ au vipengee vya uamuzi, nyota yake imeng’ara tena kutokana na kitabu hicho ambacho amekitumia kutetea sera yake ya vita dhidi ya ugaidi na uvamizi wa Iraq mwaka wa 2003.

Kitabu hicho ‘Decision Points’ kimetolewa baada ya ushindi wa wanachama wa chama cha Republican katika uchaguzi wa baraza la wawakilishi na kinakariri dhana ya ushindi baada ya kukosa udhibiti wa kisiasa kwa miaka minane ya utawala wa Bw Bush.

Kwa kipindi kirefu kijacho, rais huyo wa zamani atakuwa akionekana sana katika vyombo vya habari, hasa baada ya kuwa kimya tangu alipomkabidhi rais Obama, ufunguo wa ikulu mwezi Januari mwaka wa 2009. Lengo lake kuu litakuwa kukipigia debe kitabu chake ambacho tayari kina nakala milioni 1.5 zilizochapishwa.

Katika kurasa za kitabu hicho, ‘Decision points’ Bw Bush ameandika kuhusu makosa aliyofanya katika kampeni ya vita vya Iraq na kushindwa kwake kuzipata silaha za maangamizi makubwa ambazo duru za ujasusi za kimataifa zilitaja kwamba rais wa Irak wakati huo, hayati Saddam Hussein, alikuwa amezificha.

Kulingana na sehemu fupi kutoka katika kitabu hicho, kilichoangaziwa na televisheni ya NBC nchini Marekani, Bw Bush alinukuliwa akisema kwamba hakuna yeyote aliyepigwa na butwaa au kukasirika zaidi yake baada ya wao kukosa silaha hizo za maangamizi makubwa. Anasema alikuwa na hisia za ugonjwa kila mara alipolifikiria jambo hilo na kwamba bado ana hisia hizo.

Alipoulizwa ikiwa anazingatia kuomba msamaha kutokana na makosa hayo, Bw Bush alisema hajalifikiria suala hilo. Alisema kuomba msamaha kutakuwa na maana kwamba uamuzi uliochukuliwa ulikuwa na kasoro. Rais huyo wa zamani anatarajiwa kushiriki katika mahojiano katika kipindi cha televisheni cha jukwaa la Oprah Winfrey.

Bw Bush amesema haamini uamuzi huo ulikuwa na kasoro na kwamba la muhimu ni kuchimbua kwa nini yalitokea, nini kilichokwenda mrama na kutafuta suluhu.

Kwa ujasiri, George W Bush amesisitiza kwamba ulimwengu uko bora zaidi bila ya Saddam Hussein kuwa madarakani kwa sababu raia milioni 25 wa Iraq wanaweza kuishi kwa uhuru.

Tofauti na hayo Bw Bush aliitetea mbinu ya kuwazamisha washukiwa wa ugaidi majini akisema mbinu hiyo ya kupata habari, ilisaidia katika kusitisha mashambulio yaliyolenga uwanja wa ndege wa Hearthrow nchini Uingereza. Hayo ni kwa mujibu wa mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la The Times.

Flash-Galerie 5 Jahre Hurrikan Katrina

Bw Bush anakiri kwamba hakulishughulikia janga la Katrina kwa ustadi na alilaumiwa kwa ubaguzi wa weusi.

Kitabu cha ‘Decision Points’ kinaangazia maamuzi 14 tofauti yaliyochukuliwa na rais huyo wa zamani alipokuwa katika Ikulu na kinatoa uchambuzi wa jinsi alivyoyaafikia katika jitihada za kutoa mwangaza zaidi juu ya uongozi wake.

Mada zinazoangaziwa ni uvamizi wa kigaidi wa Septemba 11, 2001 katika miji ya New York na Washington na pia mzozo wa kiuchumi.

Bw Bush anakiri kwamba hakulishughulikia mkasa wa kimbunga cha Katrina kwa ustadi. Mwanamuziki, Kanye West aliukosoa utawala wa Bush ulivyopuuza janga la Katrina akisema uliwabagua weusi na rais huyo anajutia kwamba mtazamo huo uliomtaja pia kama mbaguzi wa rangi, ndio ulimuudhi sana wakati wa utawala wake.

Mwandishi: Peter Moss /AFP

Mhariri: Josephat Charo.

 • Tarehe 10.11.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/Q3fz
 • Tarehe 10.11.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/Q3fz

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com