1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza mikononi mwa Hamas

Ramadhan Ali15 Juni 2007

Chama cha Hamas kimeudhibiti barabara mwambao wa gaza wakati mahasimu wao Fatah wamejizatiti ukingo wa magharibi.Rais Abbas atangaza kuvunjwa kwa serikali na uchaguzi mpya kufanywa.

https://p.dw.com/p/CB3a
Hamas yadhibiti Gaza
Hamas yadhibiti GazaPicha: AP

Wanamgambo wa Hamas wakishangiria, wameudhibiti barabara mwambao wa Gaza leo na hivyo, wameunda eneo la utawala wa kiislamu mpakani na Israel.Hii inafuatia ushindi wao dhidi ya vikosi vya Al Fatah ,wapinzani wao baada ya mapigano ya siku kadhaa.

Magazeti ya Israel yameangua vilio leo kwa ushindi wa Hamas huko Gaza-yakidai ile ndoto ya msiba mkubwa sasa imetimilia.

Chama cha kiislamu cha Hamas kinachoitwa ni cha kigaidi na Israel pamoja na washirika wake wa magharibi,kimeudhibiti barabara mwambao wa Gaza masaa machache baada ya kiongozi wa FATAH na rais wa Palestina Mahmud Abbas kuivunja serikali ya Mamlaka ya ndani ya waplestina kati ya chama chake na Hamas na kutangaza hali ya hatari.

Abbas amemtimua madarakani waziri-mkuu Ismail Haniya ambae amebisha kuuzuliwa kwake.

Katibu wa rais Mahmud Abbas, Tayeb Abdel Rahman

akisoma tangazo la rais Abbas alisema zaidi :

“Mara tu hali ikitulia ,uchaguzi mpya utaitishwa .Hadi hapo Baraza la mawaziri la mpito litaendesha shughuli za serikali.”

Akijibu waziri mkuu Haniyeh kutoka chama cha Hamas alisema rais Abbas amechukua uamuzi haraka .Serikali inabakia pale pale haikuvunjwa. Uamuzi wa rais Abbas ambao umetokana na shinikizo la Marekani na Israeli,alisema, hauna maana.

Gaza imedhibitiwa kikiamilifu na chama chake Hamas na wanamgambo wake jana waliiteka kambi ya mwisho ya majeshi ya Palestina.Baadae wakamnyonga hadharani mbele ya kamera amirijeshi wa chama cha FATAH.

Ulipoingia usiku wa manane wanamgambo wa kiislamu wa Hamas wakaitia nguvuni ikulu ya rais wa palestina huko Gaza na hapo tena mwambao mzima wa gaza uko chini ya chama cha Hamas.

Wakereketwa wa Hamas na wafuasi wao wakaanza kusherehekea ushindi wa vikosi vya hamas dhidi ya Fatah.Mama mmoja alisikika akisema:

“Allah Akbar-Mungu Mkubwa.Nimeona vipi kikosi cha Hamas cha Kassam-Brigade kilivoiteketeza idara ya ujasusi.Mungu mkubwa na ninayaosema ni ukweli.Sasa risasi zielekezwe dhidi ya Marekani na Israel.”

Nini muitiko wa Israel ?

Wakati Ukingo wa magharibi umo mikononi mwa wapinzani wa Hamas-chama cha Al Fattah,magazedti ya Israel yameangua kilio kudai mtafaruku umezuka,moto na msiba mkubwa kutokana na ushindi wa hamas huko Gaza:

Gazeti la MAARIV: lilijitokeza leo na kichwa hiki cha maneno: “Ndoto ya kuzuka msiba mkubwa imedhihirika-Hamas inaudhibiti mwambao wa Gaza.Fatah imeuzuwia Ukingo wa magharibi.”

Kichwa chengine cha maneno kinasoma hivi:

“Nchi 3 zimeibuka kwa wananchi wa makabila 2.”

Gazeti hili likachapisha ramani ya Israel iliozungukwa na dola 2 za kipalestina-ile ya mashariki imepandisha bendera ya Palestina na ile ya magharibi inapepea bendera ya kijani ya chama cha Hamas.

Gazeti maarufu sana la Israel “Yediot Ahranot” limechapisha picha ya mtu alieshika bunduki akifunika uso, mkono mmoja akishika kuran akisimama juu ya meza afisini mwa rais Mahmud Abbas huko Gaza.Akinadi “ HII HAPA NI HAMASTAN”-dola la Hamas.