1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatakiwa kuondoa vizuizi

Liongo, Aboubakary Jumaa21 Januari 2008

Rais wa Mamlaka ya wapalestina Mahamoud Abbas ameitaka Israel kuondoa vikwazo ilivyoweka dhidi ya Gaza vilivyopelekea uhaba mkubwa wa nishati ya petroli.

https://p.dw.com/p/CvDB
Watoto wa Kipalestina wakisoma kwa kutumia karabai kutokana na kukosekana kwa umeme kwenye eneo hilo.Picha: AP

Uhaba huo umesababisha  kufungwa kwa mtambo pekee wa kuzalisha umeme kwenye ukanda wa Gaza.


Kufungwa huko kumepelekea eneo lote la Gaza kuwa katika gaza na kuzikwaza shughuli kadhaa za kijamii, hali inayotishia kutokea kwa janga kubwa la kibinaadamu.


Rais huyo wa Palestina ameitaka Israel kuondoa vizuizi hivyo ili kuokoa maisha ya watu wasiyo na hatia, na kuruhusu kuendelea kwa huduma za afya.


Msemaji wa Bwana Abbas, Nabil Abu Runeida ameonya kuwa iwapo Israel haitoondoa vikwazo hivyo katika muda wa saa chache zijazo watalifikisha suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.


Aidha ametaka kuitishwa kwa  mkutano wa dharura wa mawaziri wa nje wa umoja wa nchi za kiarabu kujadili juu ya mzozo huo.


Ukanda Gaza toka Alhamisi wiki iliyopita umekuwa katika giza, baada ya Israel kufunga mpaka wake na eneo hilo ikiwa ni kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya makombora yanayorushwa kutokea Gaza.


Msemaji huyo wa Rais wa Mamlaka ya Palestina amewataka Hamas kuacha mashambulizi ambayo yanawapa sababu Israel kuendelea na uvamizi,mashambulizi, na vizuizi dhidi ya wapalestina.


Mashirika ya Umoja wa Mataifa na makundi ya haki za binaadamu dunia yamelaani hatua hiyo ya Israel, lakini Israel kwa upande wake imesema kuwa wakulaumiwa ni wapiganaji wa kipalestina wanauvurumisha maroketi kutokea Gaza kila siku.


Kufungwa kwa mpaka huo kumezuia kuingizwa Gaza nishati ya Petroli inayotumika katika mtambo pekee wa kuzalishia umeme kwenye eneo hilo.


Msemaji wa  wizara ya afya ya palestina Dr Moaiya Hassanain ameonya kuwa uhaba huo wa mafuta utapelekea hathari kubwa katika sekta ya afya.


Hapo jana mamia ya wapalestina wakiwa na mishumaa waliandamana katikati ya mji wa Ramallah kwenye ukingo wa Magharibi kuonesha mshikamano wao dhidi ya wenzao wa Gaza.


Eneo hilo la ukingo wa Magharibi liko chini ya chama cha Fatah, wakati ambapo Gaza linadhibitiwa na Hamas.